Loading...

Yanga yaishushia kichapo cha goli 4 - 0 klabu ya Ndanda FC.

Wachezaji wa Yanga wakishangilia goli.
MABINGWA watetezi, Yanga SC wamejirudisha jirani kabisa na Simba SC baada ya ushindi wa mabao 4-0 jioni ya jana katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzaia Bara.

Yanga SC inafikisha pointi 40 baada ya ushindi wa jana na sasa inazidiwa pointi moja na watani wao, Simba SC ambao hata hivyo wana mchezo mmoja mkononi na watacheza na Ruvu Shooting kesho.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Eric Onoca wa Arusha aliyesaidiwa na Michael Mkongwa wa Njombe na Janeth Balama wa Iringa, hadi mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa mabao 3-0.

Mshambuliaji Mzimbabwe Donald Dombo Ngoma alifunga mabao mawili mfululizo kabla ya Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe kufunga la tatu na beki Mtogo, Vincent Bossou akafunga la nne kipindi cha pili. 

Ngoma alifunga bao la kwanza dakika ya nne akimalizia kona ya Haruna Niyonzima na akafunga la pili dakika ya 21 akimalizia krosi ya Juma Abdul Jaffar.
Mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Tambwe akaifungia Yanga bao la tatu dakika ya 25 kabla ya kuonyeshwa kadi ya njano kwa kwenda kukipiga teke kibendera cha kona wakati akishangilia bao lake.

Kipindi cha pili, Yanga ilirudi kwa kujiamini zaidi na kuanza kucheza kwa utulivu ikimiliki mpira zaidi na kuwapoteza kabisa wapinzani.

Pamoja na hayo, Yanga ililazimika kusubiri hadi zikiwa zimesalia dakika mbili ili kupata bao lake la mwisho, lililofungwa na Bossou kwa kichwa akimalizia kona ya beki wa kulia, Juma Abdul Jaffar.

⁠⁠Kikosi cha Yanga kilikuwa na wachezaji hawa wafuatao; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Hajji Mngwali, Vincent Bossou, Kevin Yondan, Said Juma ‘Makapu’/Justine Zulu dk60, Simon Msuva, Haruna Niyonzima/Thabani Kamusoko dk70, Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Emmanuel Martin/Geoffrey Mwashiuya dk77.

Ndanda FC; Jeremiha Kisubi, Kiggi Makassy, Bakari Mtama, Paul Ngalema, Hemed Khoja, Salvatory Ntebe/Ayoub Shaaban dk40, Abuu Ubwa/Salum Minely dk53, Nassor Kapaman Salum Telela, Omar Mponda na Riffat Khamis.

ZeroDegree.
Yanga yaishushia kichapo cha goli 4 - 0 klabu ya Ndanda FC. Yanga yaishushia kichapo cha goli 4 - 0 klabu ya Ndanda FC. Reviewed by Zero Degree on 12/29/2016 12:13:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.