Aboud Jumbe aacha ujumbe mzito.
Jumbe, ambaye alivuliwa nyadhifa zote serikalini na ndani ya CCM kutokana na kutofautiana na chama hicho katika suala la muundo wa Muungano, alishika nafasi ya urais mwaka 1972 baada ya muasisi wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume kuuawa katika jaribio la mapinduzi.
Akizungumzia kifo hicho, mtoto wa Jumbe Mustafa Jumbe amesema sababu ya kifo cha baba yake ni umri mkubwa ambao ni miaka 96.
Amesema kabla ya kuzikwa leo mwili, utaswaliwa katika msikiti wa Mwembeshauri na kuzikwa nyumbani kwake Migombani, Zanzibar.
“Marehemu ameacha wake wawili, watoto 14 na wajukuu zaidi ya 30,” amesema Mustafa.
Akataa kuzikwa kifahari
Mazishi ya kiongozi huyo aliyekaa madarakani kwa miaka 12 ikiwa ni muda mrefu kuliko marais wengine wa Zanzibar, yanaweza kutoshirikisha taratibu za kiserikali kutokana na wosia alioandika kabla ya kifo chake.
“Sitaki katika maziko yangu kutumbuizwa chochote kiendacho hata kidogo kinyume na mafundisho ya Islamu,” anaandika katika wosia huo.
“Sitaki beni (bendi), sitaki mizinga, sitaki maombolezo wala lolote jingine lenye hata chembe ya kufuru. Sitaki hivyo nikiwa hai, nitakapoondoka katika dunia. Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi wangu, duniani na akhera.”
Kwa kawaida kiongozi wa kada yake anapofariki, hupigiwa mizingi 21 na kusubiri taratibu za kiserikali ambazo wakati mwingine huchukua muda kukamilika tofauti na sheria za dini hiyo.
Magufuli atuma salamu
Kutokana na kifo hicho, Rais John Pombe Magufuli na viongozi wengine mbalimbali wa Serikali wametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Jumbe, wakielezea kusikitishwa na msiba huo.
Rais Magufuli ametuma salamu hizo kwa Rais wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein na kusema kuwa Taifa limempoteza mtu muhimu ambaye alijitoa kupigania uhuru, umoja, haki na maendeleo ya wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika kipindi kigumu ambacho Taifa lilikipitia.
“Nimeshtushwa sana na kifo cha mzee wetu, Aboud Jumbe. Kwa hakika Tanzania imepoteza mtu muhimu ambaye katika kipindi cha uongozi wake alitoa mchango mkubwa wa kuipigania na kuijenga Tanzania tunayoiona leo,” amesema Rais Magufuli katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Gerson Msigwa.
“Kupitia kwako Dk Shein, napenda kuipa pole familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki wote, wananchi wa Zanzibar na Watanzania wote kwa ujumla kwa kufikwa na msiba huu mkubwa.”
Mbowe amkumbuka
Akizungumzia kifo hicho, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitoa pole kwa niaba ya chama hicho kikuu cha upinzani kwa familia na Serikali ya Tanzania na Zanzibar.
Mbowe alisema serikali hizo mbili zilimtenga kwa muda mrefu kiongozi huyo kwa kile alichoeleza kuwa ni kukinzana na msimamo wa chama chake wakati wa utawala wa Mwalimu Julius Nyerere.
Alisema msimamo wa Jumbe kuhusu Zanzibar na wa chama chake ni mfano wa kuigwa.
CCM washtushwa
Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka alisema wameshtushwa na kifo cha Jumbe.
Alisema kiongozi huyo atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa wakati uongozi wake hasa wakati chama cha Afro-Shiraz (ASP) kilipoungana na Tanganyika African Nation Union (Tanu) na kuunda CCM mwaka 1977.
CUF waomboleza
Pia, CUF imetoa salamu za rambirambi kwa Wazanzibari na Watanzania wote kutokana na kifo hicho.
Mkurugenzi wa habari, uenezi na mahusiano wa chama hicho, Salim Bimany alisema wamepokea msiba huo kwa masikitiko makubwa na watamkumbuka kama kiongozi wa mwanzo baada ya Mapinduzi ya 1964 aliyefungua milango ya demokrasia kwa kuanzisha chombo cha kuwasemea wananchi wa Zanzibar ambacho ni Baraza la Wawakilishi lililoanzishwa 1980.
“Alhaj Jumbe ndiye aliyetandika misingi ya kidemokrasia Zanzibar na kuanzisha utawala wa sheria na katiba. Yeye ndiye aliyeurejesha mhimili wa mahakama uliopotea baada ya Mapinduzi kwa kuwa Zanzibar ilikuwa ikitawaliwa kwa amri za kijeshi,” alisema Bimany.
“Alipunguza makali ya mkono wa chuma, madaraka ya kiimla na kuwaondoshea hofu wananchi. Kusema kweli alijitahidi kwa mujibu wa uwezo wake na mazingira yaliyokuwapo kuhakikisha Zanzibar inapata hadhi na mamlaka yake ya kinchi. Ni mtu aliyekisimamia anachokiamini,” alisema mkurugenzi huyo wa habari wa CUF.
Sheikh asimulia
Akizungumza na na waandishi wa habari kwa njia ya simu, Sheikh Mohamed Issa wa Dar es Salaam alisema anamkumbuka Alhaj Jumbe kwa kuwa mkweli na muwazi pamoja na mitihani yote aliyoipata.
Source: Mwananchi
ZeroDegree.
ZeroDegree.
Aboud Jumbe aacha ujumbe mzito.
Reviewed by Zero Degree
on
8/15/2016 08:15:00 AM
Rating: