Loading...

Yanga SC na matarajio ya kuwashangaza watu katika mechi dhidi ya Zanaco ya Zambia

KOCHA msaidizi wa mabingwa wa soka Tanzania Yanga, Juma Mwambusi, amesema leo watawashangaza watu kwa kutoa kipigo kwa wapinzani wao Zanaco kwenye mchezo wa marudiano wa kombe la Shirikisho Afrika.

Mwambusi, alisema kuwa kikosi chake kina nafasi ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo kama tu wachezaji watafanya kile walichoelekezwa na benchi la ufundi.

"Tuko tayari kwa mchezo.., tumeweka mipango ya ushindi ambayo wachezaji wataingia uwanjani kuitekeleza na kuipa nafasi timu kusonga mbele," alisema Mwambusi.

Aidha, alisema kuwa Yanga imekuwa ikifanya vizuri kwenye michezo ya ugenini na wataendeleza rekodi hiyo kwenye mchezo wa leo unaochezwa katika Uwanja wa Taifa wa Zambia.

Yanga leo itakosa huduma ya nyota wake, Donald Ngoma na Amis Tambwe ambao wamewaacha nchini kutokana na kuwa majeruhi.

Mwambusi, alisema nyota Thaban Kamusoko na kiungo Haruna Niyonzima watakuwepo kwenye kikosi cha kwanza leo pamoja na kumtumia Obbrey Chirwa katika nafasi ya mshambuliaji wa kati.

"Mchezo uliopita Chirwa alichezeshwa pembeni lakini kesho (leo) atacheza mshambuliaji wa kati na pia Kamusoko atarejea Uwanjani," alisema Mwambusi.

Niyonzima hakucheza kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam lakini leo atakuwa miongoni mwa viungo wa timu hiyo kwenye mchezo wa leo pamoja na Deus Kaseke.
Yanga SC na matarajio ya kuwashangaza watu katika mechi dhidi ya Zanaco ya Zambia Yanga SC na matarajio ya kuwashangaza watu katika mechi dhidi ya Zanaco ya Zambia Reviewed by Zero Degree on 3/18/2017 10:42:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.