Loading...

Maagizo matatu ya Waziri Nchemba kwa jeshi la Magereza nchini

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba leo Machi 17, 2017 ametoa maagizo matatu mazito kwa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza yaliyolenga kuboresha utendaji kazi wa idara hiyo nyeti hapa nchini.

Nchemba ametoa maagizo hayo, wakati akifungua mkutano wa mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza uliofanyika katika Bwalo Kuu la Maafisa Magereza Ukonga, jijini Dar es Salaam.

Agizo la kwanza alilolitoa ni jeshi hilo kuhakikisha linadhibiti wafungwa wa makosa ya jinai hususani ya kigaidi, mauaji, visasi, na uuzwaji, usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya, kuendelea kusuka mipango ya uhalifu wawapo gerezani kwa kushirikiana na baadhi ya askari magereza wasio waaminifu.

“Muangalie namna ya kuwadhibiti wafungwa wa makosa ya jinai hasa wa dawa za kulevya, ugaidi, visasi na mauaji kutoendelea kusuka mipango ya kufanya uhalifu uraia kwa kushirikiana na mitandao ya kihalifu kwa msaada wa baadhi ya askari wasio waaminifu. Haitakuwa na maana endapo mfungwa anafungwa lakini bado anatekeleza uhalifu akiwa gereza, sababu lengo letu kuu ni kurekebisha wakosefu pamoja na kuondoa uhalifu uraiani,” amesema.

Agizo la pili alilolitoa Nchemba kwa jeshi hilo, ni matumizi mazuri ya fursa zilizopo ndani ya Jeshi la Magereza, ikiwemo matumizi mazuri ya ardhi kwa shughuli za kilimo, mifugo na hifadhi ya mazingira kwa kutumia nguvu kazi ya wafungwa katika shughuli za uzalishaji hasa uzalishaji wa chakula.

“Jeshi la Magereza lina ardhi takribani hekta 130,482 ambazo zinafaa kwa shughuli za kilimo, tumieni ardhi mliyonayo kuzalisha chakula kwa kuwa mna nguvu kazi ya kutosha, haiwezekani serikali ipoteze pesa kwa ajili ya kununua chakula cha wafungwa wakati wao wana uwezo wa kulima chakula chao. Inatakiwa walime ili kipatikane chakula cha kutosha kwa ajili ya kulisha walio uraiani hasa wanafunzi katika shule za bweni za serikali,” amesema.

Aidha, Nchemba amelitaka jeshi hilo kuondoa migogoro ya ardhi baina yake na wananchi, kwa kupima maeneo yake ya ardhi na kuwa na hati, kuweka mipaka katika maeneo hayo kwa kupanda miti na kuyafanyia ukaguzi wa mara kwa mara.

Agizo la mwisho alilolitoa, Jeshi hilo kuweka mikakati thabiti ya kutatua changamoto zinazokwamisha utendaji kazi wake pamoja na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya chombo hicho.

Naye Kamishna Jenerali wa Magereza Dkt. Juma Malewa, amemuahidi Waziri Nchemba, kuwa watautumia vyema mkutao huo, kupanga mikakati itakayowezesha kuboresha utendaji kazi wa jeshi hilo.
Maagizo matatu ya Waziri Nchemba kwa jeshi la Magereza nchini Maagizo matatu ya Waziri Nchemba kwa jeshi la Magereza nchini Reviewed by Zero Degree on 3/18/2017 10:36:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.