Fumanizi la Mapenzi: Sehemu ya 03
Ilipoishia..........Mwadawa alianza kubadilika taratibu kitabia mpaka wanajamii walishtushwa na mabadiliko ya haraka ya msichana huyo aliyekuwa akihusudu ngono kama ubweche kwa watoto. Kubadilika kwa Mwadawa kulimfanya atabiliwe kwa mambo mengi sana likiwemo la kufika mbali sana kielimu. Mitihani ilfanyika na matokeo yalipotoka jina langu la David Sikitiko lilikuwa la kwanza juu kabisa na la Mwadawa kusomeka kwenye namba kumi na moja. Familia zetu na za wanafunzi wengine waliochaguliwa zilikuwa na furaha isiyo ya kifani.
*******
Ikiwa ni miezi mine tangu tuchaguliwe kujiunga na kidato cha kwanza, siku moja zilizagaa taarifa za kuwepo kwa sherehe za kuwakaribisha wanafunzi wa kidato cha kwanza alimaarufu kama “Welcome form one”. Taarifa hizo zilizokuwa si rasmi zilipokelewa kwa furaha kubwa sana na baaadhi ya wanafunzi hasa wale wa vidato vya juu. Kwa upande wangu sikuwa na mshawasha juu ya jambo hilo kwani malezi niliyokulia vitu kama hivyo havikuwa damuni kitu ambacho wenzangu waliniweka kwenye kundi la watumishi wa Mungu au washamba kama baadhi ya vijana walivyokuwa wakitubatiza au kutusilimisha majina yasiyo rasmi kiimani. Taarifa za sherehe hiyo zilienea kama moto wa petrol kwenye nyasi kavu za kiangazi na kuwa gumzo kuu la wiki hapo shuleni kwetu kwani kila kona ambapo ungewakuta wanafunzi wawili au zaidi, mjadala ambao ungeusikia ni wa “Wellcome form one” na namna sherehe hiyo inavyofaa kwa wanafunzi. Siku zote waswahili huwa na misemo yao mingi sana lakini mimi najikita kwenye usemi huu usemao, “Kila shetani na mbuyu wake” na hivi ndivyo ilivyokuwa kwa upande wangu kwani si kama nilijitenga sana na vijana wenzangu watukutu na wakorofi bali nilikuwa karibu nao sana ili nijifunze nisiyoyajua niyajue na kufanya mikakati ya namna ya kusaidiana nao kimitazamo na misimamo kwa kuwa na mfumo mzuri wa kimaadili kwa vijana wote wa kitanzania.
*******
Miongoni mwa marafiki zangu kuna mmoja ambaye sikupenda kuwa mbali naye ni huyu wa kidato kimoja aliyekuwa anaitwa Mohamed Kitope alimaarufu kama “Mood”, kijana mjanja toka maeneo ya Sultani mkoani Morogoro. Kijana huyu tulipendana sana kwani vipaji vyetu viliendana sana kama vile kupenda shule, fani za ndani, maigizo, ngoma za asili bila kusahau uchaji Mungu. Utofauti wetu ulikuwa mdogo sana kwani yeye alikuwa mtu wa ‘totozi’ na pia alikuwa ni mpenzi wa disko wakati mimi nilikuwa kama padre nisiye na kanisa maalumu kwani niliwaona ‘totozi’ wote kama dada zangu au mama zangu. Rafiki yangu huyu alikuwa ni mtu wa ‘comedy’ sana kama mimi jambo ambalo lilitufanya tupendwe na watoto wa kike ambao walikuwa ni wanafunzi wa kutwa katika shule yetu. Kupendwa kwetu na watoto wa kike kwangu mimi niliitafsiri kama upendo wa agape wakati mwenzangu aliupokea kama upendo wa malavidavi wa kuoneana haya kwa kufanya mabaya na bila haya kijana mood alinifundisha mengi ambayo sikuyachukua yote kwani wafasihi husema, “Akili ya kupewa changanya na ya kwako.” Tukiwa bwenini alinihadithia mambo mengi yahusuyo utamu kolea upatikanao kwenye tunda la mti wa katikati hasa ukimpata Yule ajuae kugawa dozi kwa raha bila karaha. Kwa kuwa nilikuwa mshamba wa mapenzi niliyeaminishwa kuwa utamu wa kitu upo kwenye vionjo vya ulimi, nilimuona huyu rafiki yangu kama msimuliaji wa hadithi za ndoto za alinacha kutaka kujenga nyumba hewani. Siyo kama simulizi zake zilinichosha bali nyingine zilikuwa na umuhimu mkubwa juu ya maisha yangu. Kikubwa alichowahi kunichekesha ni kile cha kuingia kwenye mechi na timu kubwa bila maandalizi na limama lijuvi la mji katika “guest bubu” maeneo ua kilakala, kitendo kilichomsababishia ajikute akizindukia kwenye wodi ya wagonjwa mahututi katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro huku matone ya ‘drip’ yakishindana kuingia kwenye mwili wake kwa lengo la kuyapandisha mapigo ya moyo wake yaliyokuwa yamepoteza welekeo. Aliponisimulia kisa hicho, kwa uhakika nilicheka sana mpaka moyo ulijiachia wenyewe pasina kujielewa lakini nilijiuliza moyoni, Mapenzi ni kitu gani mpaka yanawafanya watu kuwa hivyo? Majibu sikuyapata kwa uzuri zaidi.
*******
====>>Itaendelea wiki ijayo...
Usiikose SEHEMU YA 04>>> ya Riwaya hii ifikapo jumatatu ya wiki inayofuata, na utaipata hapa Zero Degree pekee.
Fumanizi la Mapenzi: Sehemu ya 03
Reviewed by Zero Degree
on
6/09/2017 12:33:00 PM
Rating: