Loading...

Mahakama 'yamweka kiporo' Prof. Lipumba


HATIMA ya Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), kuendelea au kutenguliwa kushika wadhifa huo, sasa itajulikana Machi 17, mwaka huu, baada jana kupigwa kalenda katika Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.

Uamuzi wa hatima hiyo ulipangwa kusomwa jana kutokana na kesi iliyofunguliwa na Bodi ya Baraza la Wadhamini la CUF dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Lipumba, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wengine 11 mbele ya Jaji Benhajj Masoud.

Mapema mwaka 2016, walalamikaji waliwasilisha maombi kupitia mawakili Juma Nassoro na Daima Halfan wakitaka mahakama kumvua nafasi hiyo Profesa Lipumba baada ya kuwasilisha barua kwa msajili wa vyama vya siasa kujitoa katika wadhifa huo.

Jana Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Sharmillah Sarwatt, alisema kesi hiyo ilipangwa kusomwa uamuzi lakini jaji aliyepangiwa kusikiliza amepata udhuru wa kikazi.

Msajili alisema uamuzi huo utatolewa Machi 17, mwaka huu (kwa mujibu wa kalenda ya mwaka 2019, siku hiyo itakuwa Jumapili). Wadaiwa wengine katika kesi hiyo namba 23 ya mwaka 2016 ni viongozi 10 wanaomuunga mkono, akiwamo Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Madgalena Sakaya.

Katika maombi ya msingi, Bodi ya Wadhamini imeiomba mahakama itoe amri ya kubatilisha barua ya Msajili inayomtambua Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti wa CUF, wakidai kuwa hana mamlaka na imzuie kuingilia masuala ya ndani ya kiutawala ya chama hicho.

Ilidaiwa kuwa Profesa Lipumba alishajiuzulu nafasi hiyo na katiba ya CUF haina utaratibu wa kiongozi kujiuzulu na kutengua tena uamuzi wake huo na kurejea katika nafasi yake na kwamba si mwanachama kwani alishavuliwa uanachama.

Hata hivyo, Profesa Lipumba anadai kuwa kwa mujibu wa Katiba ya CUF, ibara ya 117 (2) mchakato wa kujiuzulu kwake ulikuwa bado haujakamilika.

Pia anadai ili uamuzi wa kujiuzulu ukamilike, ni lazima mamlaka ya uteuzi wake (mkutano mkuu wa Taifa wa chama) ukae na kuridhia au kukataa.

Chanzo: Nipashe
Mahakama 'yamweka kiporo' Prof. Lipumba Mahakama 'yamweka kiporo' Prof. Lipumba Reviewed by Zero Degree on 2/23/2019 08:05:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.