Chadema walaani Sugu kukamatwa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimelaani kitendo cha Jeshi la Polisi kumkamata Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ kwa tuhuma za kutoa kauli za uchochezi.
Mbunge huyo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema jana Februari 21, aliitikia wito wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai ambao kwa nyakati tofauti walimtaka afike Kituo Kikuu cha Polisi kwa mahojiano kuhusu kauli alizozitoa Jumamosi Februari 16, wakati akizungumza na wananchi wa jimbo lake baada ya kutoa misaada ya vifaa vya ujenzi katika Shule ya Msingi Ikuti kama alivyowaahidi.
Sugu alishikiliwa kituoni hapo kwa saa kadhaa kisha kuachiliwa kwa dhamana saa 12 jioni na kutakiwa kuripoti tena leo kituoni hapo kwa mahojinao zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Ijumaa Februari 22, Naibu Katibu Mkuu Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu amesema wanalaani kwa sababu Sugu amekamatwa wakati akiwa katika majukumu yake kwa mujibu wa katiba.
Mwalimu amesema Sugu alikuwa akijibu kero mbalimbali za wananchi wake ambapo aliwaahidi watakwenda kuhoji bungeni suala la wamachinga kuuziwa vitambulisho.
“Sugu alihoji kwanini vitolewe vitambulisho elfu 45 wakati wamachinga wako 25,000 vitakavyobaki vinaenda wapi kama siyo kwenda kugawiwa kiholela mtaani, wangemuacha akahoji bungeni kisha serikali imjibu.
“Katika video iliyosambaa jana RPC akielezea kitu gani kimewafanya wamshikilie Mbunge huyo, alisema aliyoyaongea yanaweza kuleta uchochezi na kuhatarisha usalama na waliandaa mkutano huo bila kuwapa taarifa jeshi la Polisi.
“Tunamtaka RPC aje atuelezee ni sheria ya wapi inamtaka Mbunge kuomba ruhusa Polisi ili aongee na wananchi wake na lini imekuwa kosa kuikosoa serikali, Sugu alisema mradi huo umefanyika bila kushirikisha wadau na ni kweli kwasababu haiwezekanu upeleke vitambulisho bila kujua idadi ya wanaovihitaji,” amesema.
Chanzo: Mtanzania
Chadema walaani Sugu kukamatwa
Reviewed by Zero Degree
on
2/23/2019 07:50:00 AM
Rating: