Loading...

Mwandishi wa Habari wa ITV aachiwa kwa dhamana.

Mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha ITV mkoani Arusha, Khalfan Lihundi (katikati), akizungumza na waandishi wa habari nje ya Kituo cha Polisi cha Usariver, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha baada ya kuachiwa kwa dhamana jana baada ya kushikiliwa kwa zaidi ya saa 24 akidaiwa kuandika habari za migogoro ikiwamo ya ardhi na maji wilayani humo.
HATIMAYE mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha ITV mkoani Arusha, Khalfan Lihundi, ameachiwa kwa dhamana jana baada ya kuhojiwa.

Lihundi aliachiwa jana saa 9:20 alasiri baada ya kuwekwa rumande kwa zaidi ya saa 24 tangu juzi Desemba 21, mwaka huu saa 8 mchana katika kituo cha Polisi cha Usa river, wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha.

Aliwekwa rumande kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti, aliyedai kuwa amekuwa akiandika habari za uchochezi.

Baada ya mwandishi huyo kuachiwa, shangwe zilitawala kutoka kwa wanahabari wenzake wa Mkoa wa Arusha ambao walifika kituoni hapo kujua hatima yake.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuachiwa kwa dhamana, Liundi alisema katika mahojiano kati yake na polisi alidaiwa kuripoti habari za migogoro ya ardhi na maji ambazo hazikumfurahisha DC Mnyeti.

“Habari nyingine ninazodaiwa kuripoti ni za kipindi cha wakuu wa wilaya waliopita, ambazo nyingi ni za migogoro ya wananchi, hivyo inaonekana taarifa za wananchi hazitakiwi wakati taarifa nyingi hata Rais John Magufuli, anaziona kwenye vyombo vya habari na kutolea uamuzi ikiwamo suala la wamachinga.

“Sijajengewa hofu, nasikia natafutwa hata Wilaya ya Ngorongoro na nitakwenda, nitawekwa ndani hata mara 200, lakini sitaogopa wala kurudi nyuma, kwani taarifa hizo nyingi huwa kuna viongozi kama madiwani na wenyeviti wa vijiji, ila naona hawaruhusiwi kuongea zaidi ya uongozi wa wilaya,” alisema

Aliwataja wakuu hao wa wilaya waliopita ambao anadaiwa katika kipindi chao alikuwa akiripoti habari hizo za uchochezi kuwa ni Hasna Mwilima ambaye hivi sasa ni Mbunge wa Kigoma Kusini kupitia CCM na Wilson Nkumbaku aliyetenguliwa uteuzi wake na Rais Magufuli.

“Nawashukuru waandishi wenzangu kwa ushirikiano huu kwani suala hili halikwepeki, mwandishi yeyote anaweza kuwekwa ndani na nitaripoti taarifa yoyote kwani kila ngazi ya uongozi inahusika na wangekuwa hawatakiwi wasingekuwapo kisheria,” alisema.

ZeroDegree.
Mwandishi wa Habari wa ITV aachiwa kwa dhamana. Mwandishi wa Habari wa ITV aachiwa kwa dhamana. Reviewed by Zero Degree on 12/23/2016 12:35:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.