Loading...

Yanga yapangiwa Wacomoro ligi ya mabingwa Afrika.

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga wamepangwa kuanza raundi ya awali ya michuano hiyo dhidi ya Ngaya de Mbe ya Comoro.

Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo iliyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), mshindi wa mechi hiyo atacheza na mshindi kati ya APR ya Rwanda na Zanaco ya Zambia.

Aidha, wawakilishi wa Zanzibar kwenye michuano hiyo, timu ya Zimamoto imepangwa kuanza na Ferroviario Beira ya Msumbiji.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Yanga wataanzia ugenini kati ya Februari 10, 11 na 12 mwakani kabla ya kurudiana Februari 17, 18 au 19.

Yanga ilishawahi kucheza na APR msimu uliopita na kuitoa kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya kuifunga mabao 2-1 katika mechi ya kwanza iliyochezwa Kigali kabla ya kutoka nayo sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Wawakilishi hao waliishia hatua ya 16 kwenye Ligi ya Mabingwa kabla ya kucheza robo fainali za Kombe la Shirikisho baada ya kuondolewa Ligi ya Mabingwa na Al Ahly ya Misri.

Wawakilishi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, Azam wamepangwa kuanza raundi ya kwanza ambapo watacheza na mshindi kati ya Mbabane Swallows ya Swaziland na Opara United ya Botswana.

Azam wao wataanzia nyumbani kati ya Machi 10, 11 au 12 na marudiano Machi 17, 18 au 19 mwakani.

Kwa upande wa Zanzibar KVZ imepangwa kuanza na Messager Ngozi ya Burundi na mshindi wa mechi hiyo atacheza na Zeso ya Zambia.

ZeroDegree.
Yanga yapangiwa Wacomoro ligi ya mabingwa Afrika. Yanga yapangiwa Wacomoro ligi ya mabingwa Afrika. Reviewed by Zero Degree on 12/22/2016 11:53:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.