Loading...

Kinachompa jeuri Vincent Bosou wa Yanga chabainika

HALI bado haijakaa vizuri kati ya beki kisiki wa Yanga, Vincent Bossou na mashabiki wa kikosi hicho, ambao wamekasirishwa na raia huyo wa Togo kukataa kucheza mchezo dhidi ya Simba, lakini tayari imegundulika mtu anayempa jeuri.

Beki huyo ameendelea kuweka mgomo wa kuichezea timu hiyo kwa madai ya kutolipwa mshahara wake wa miezi minne, ambapo baadhi ya mashabiki wanadai amechangia kikosi chao kufungwa mabao 2-1 na Simba, kwani angekuwapo huenda hayo yote yasingetokea.

Hata hivyo, wakati kila mmoja akiwa anajiuliza nini hatima ya beki huyo, imegundulika kuwa nahodha wa zamani wa timu ya Taifa ya Togo ambaye ni swahiba wake, Emmanuel Adebayor, anahusika kwa namna moja ama nyingine.

Taarifa za uhakika kutoka kwa rafiki wa karibu wa Bossou, ambaye na yeye mwenyewe amezithibitisha, zinadai kuwa, Adebayor anamtafutia timu ya kuchezea huko Ulaya na atakapomaliza mkataba wake na Yanga msimu huu hataongeza mwingine.

“Nadhani hata yeye mwenyewe ameshaweka wazi kuwa akimaliza mkataba wake hataongeza mwingine, hii inatokana na mambo yao ya chini kwa chini na Emmanuel Adebayor ambaye anahangaika kumtafutia timu ya kucheza barani Ulaya,” alisema rafiki huyo.

Alivyotafutwa beki huyo ili kuzungumzia sakala hilo, ambapo alikiri kuwa kuna mambo yake na Adebayor yanayoendelea ambayo asingependa kuyaweka wazi kwa sasa.

“Kwa sasa ninapumzika nyumbani, masuala yote ninamuachia Mungu, kuhusu hilo la kaka yangu Adebayor nisingeweza kuzungumza lolote kwa sasa, ila niseme tu kwamba ni mtu ambaye tunazungumza sana na anajua siri zangu,” alisema.

Akizungumzia kwanini amesusa kuichezea Yanga katika mchezo dhidi ya Simba mwishoni mwa wiki iliyopita, alisema anaidai timu hiyo mshahara wa miezi mitatu na atakapolipwa hakuna shaka kwamba atajumuika na wenzake.

“Kama nilivyosema bado nipo nyumbani tu napumzika, nina madai yangu ya mshahara wa miezi mitatu, ikiwamo Agosti, Desemba pamoja na Januari na wananizungusha tu, kama wakinipa haki yangu nami nitafanya kazi iliyonileta hapa Tanzania,” alisema.

Akizungumzia mkabata wake na timu hiyo, alisema unamalizika msimu huu na kwa hali ilivyo ni vigumu kuongeza mwingine, huku akidai kuwa, utakapokwisha ndipo anaweza kutoa jibu la moja kwa moja.

Katika hatua nyingine, baada ya beki huyo kudai kuwa anaidai klabu mshahara wa miezi mitatu. Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa alitafutwa, ambapo alisema siyo kweli kwamba Muivory Coast huyo anaidai timu mshahara wa miezi mitatu, badala yake ni mwezi huu tu na kwamba wanasikitika jinsi anavyoichafua timu mitandaoni.

“Kwanza ametumia njia isiyo sahihi kuichafua klabu kwenye mitandao ya kijamii, tumemwita aje kueleza kwanini anazungumza vitu asivyokuwa na ushahidi navyo, alishaandikiwa hundi yake, lakini hatukuweza kumpa mtu mwingine zaidi yake, haidai klabu pesa yoyote zaidi ya mshahara wa mwezi huu ambapo wachezaji wote wanadai pia,” alisema Mkwasa.

Source: DIMBA
Kinachompa jeuri Vincent Bosou wa Yanga chabainika Kinachompa jeuri Vincent Bosou wa Yanga chabainika Reviewed by Zero Degree on 3/01/2017 09:55:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.