Loading...

Unaikumbuka ishu ya mama aliyedai kuibiwa kichanga hospitali ya Temeke? Hivi ndivyo ilivyoisha!

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RMO), Dk Grace Magembe amekamilisha uchunguzi wa sakata la mama anayedai kuibiwa mmoja wa watoto mapacha alipojifungua kwa upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke.

Juzi, Dk Magembe aliitisha kikao katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambacho kilimalizika usiku.

Kikao hicho kiliitishwa kutokana na madai yaliyotolewa na Asma Juma (29) na mumewe Abubakari Pazi wakazi wa Mbande wilayani Temeke kwamba, mtoto wao mmoja aliibwa.

Inadaiwa kuwa kikao hicho kiliwahusisha walalamikaji na wanafamilia, madaktari waliomfanyia upasuaji mama huyo na wahudumu waliohusika kumhudumia katika hatua mbalimbali tangu akihudhuria kliniki katika zahanati ya Serikali iliyopo Mbande.

Akizungumzia jambo hili jana, Dk Magembe alisema kikao hicho kilifanyika hadi saa nne usiku na kwamba, amebaini kilichotokea na kuahidi kutoa taarifa kwa vyombo vya habari baada ya kumaliza kuandika taarifa ya suala hilo.

“Tulimaliza kikao saa nne usiku Alhamisi, nisingeweza jana (Ijumaa) kumaliza kuandika ripoti, ila nimejua kilichotokea na taarifa ikiwa tayari mtaitwa wote (vyombo vya habari) na mtasomewa siyo kwamba atapewa mmojammoja,” alisema. 

Dk Magembe aliingilia kati sakata hilo baada ya kuelekezwa na Naibu Waziri wa Afya, Dk Hamisi Kigwangalla ili kupata ukweli wa tuhuma zilizotolewa na wanandoa hao.

Asma anadai kuibiwa mtoto alipojifungua kwa upasuaji Aprili 19, baada ya kupewa dawa iliyomfanya apoteze fahamu muda mfupi baada ya kuanza kufanyiwa upasuaji.

Anadai vipimo vya ultrasound alivyofanyiwa mara mbili akiwa mjamzito vilionyesha alikuwa ana mimba ya mapacha na kwamba, hata siku alipofika Hospitali ya Temeke alifanyiwa vingine vya kawaida na madaktari wawili ambao walibaini alikuwa na mapacha, lakini mtoto mmoja alikuwa amekaa vibaya ndipo ikabidi afanyiwe upasuaji.

Mzazi huyo anadai kuwa alipoingizwa katika chumba cha upasuaji, alichomwa sindano ya ganzi na baada ya kuanza kufanyiwa upasuaji alipatiwa dawa nyingine kupitia mrija wa chupa ya maji aliyowekewa mkononi (drip).

Baada ya hapo anadai hali yake ilianza kubadilika na kisha kupoteza fahamu kiasi kwamba hakujua kilichoendelea hadi alipozinduka na kujikuta kwenye chumba kingine na kesho yake ndipo alipokabidhiwa mtoto mmoja.
Unaikumbuka ishu ya mama aliyedai kuibiwa kichanga hospitali ya Temeke? Hivi ndivyo ilivyoisha! Unaikumbuka ishu ya mama aliyedai kuibiwa kichanga hospitali ya Temeke? Hivi ndivyo ilivyoisha! Reviewed by Zero Degree on 5/01/2017 12:36:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.