Loading...

Mbunge wa CCM aiomba Serikali iwakamate Chenge na Ngeleja


MBUNGE wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Musukuma, ameiomba serikali iwakamate wabunge wa CCM waliotajwa kwenye kashfa ya kusafirisha mchanga wa dhahabu, maarufu kama makinikia, nje ya nchi.

Amesema wabunge hao William Ngeleja (Sengerema), Andrew Chenge (Bariadi Mashariki) na Dk. Dalali Kafumu (Igunga), wanapaswa kukamatwa kwa kuwa hawana kinga inayozuia serikali kuwatia nguvuni.

Musukuma aliyasema hayo jana wakati akichangia mjadala wa Bajeti ya 2017/2018, ambapo alisema kwa muda mrefu serikali imekuwa ikipata wakati mgumu kwenye kashfa mbalimbali zilizotokana na wabunge hao ambao wako kwenye chama tawala.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, hao watu wanaotajwa tunao humu humu na hawana kinga. Kwa nini sasa wasikamatwe?" Alihoji Musukuma. 

"Kuna mwingine yuko humu baada ya kutajwa kaandika kwenye (mtandao wa kijamii) twitter kuwa hawezi kuhojiwa hadi atakapofikishwa mahakamani.

"Sasa mtu ametuhumiwa halafu anatamba kwenye mitandao ya kijamii kana kwamba ana kinga. Hii si sahihi.” 

Aidha, Msukuma alisema kuna wabunge wa CCM ambao wamekuwa wakitajwa kwenye kashfa mbalimbali zinazotokea, lakini hawajachukuliwa hatua.
Aliishauri serikali kwa kuwa wabunge watatu hao walitajwa kwenye ripoti alizokabidhiwa Rais John Magufuli hivi karibuni wakamatwe.

“Mheshimiwa Mwenyekiti kuna mbunge humu kila kashfa anatajwa yeye, kila tuhuma inayotajwa yumo. Ana kinga gani huyu? Kwa nini asikamatwe?" Alisema Musukuma. 

"Hili suala tusilichukulie kimzaha mzaha na wala tusiigeuze CCM kuwa pango la watu wenye tuhuma kujificha.

"Lazima wakamatwe hawa ili iwe mfano kwa wengine.” 

Ripoti iliyowasilishwa Jumatatu na mwenyekiti wa kamati maalum iliyochunguza masuala ya sheria na kiuchumi kuhusiana na makinikia, Prof. Nehemia Osoro ilisema nchi inaweza kuwa imepoteza mpaka Sh. trilioni 489 katika kodi na mali (madini) kwa miaka 19 iliyopita kwenye biashara hiyo ya madini inayofanywa na Acacia. Kati ya fedha hizo, kiwango cha kodi kilitajwa kuwa Sh. trilioni 108.

Kamati hiyo iliyoundwa na Rais John Magufuli Aprili 10 ikiwa na wajumbe nane wabobezi katika sheria, takwimu na uchumi iligundua kwa kima cha chini, nchi imepoteza Sh. trilioni 252 kupitia usafirishaji wa makinikia.

Aidha, kamati hiyo ilisema hasara hiyo ingeweza kuepukika kama kungekuwa na umakini miongoni mwa watumishi wa umma waliokuwa kwenye nyadhifa za uwaziri wa nishati na madini, wanasheria wakuu wa serikali, makamishna wa madini na wengine kwenye mlolongo huo kati ya 1998 na mwaka huu na kushauri wahojiwe.

Wakati Ngeleja amepata kuwa Waziri wa Nishati na Madini katika kipindi hicho, Chenge alikuwa Mwanasheria Mkuu na Kafumu Kamishna wa Madini.

Wakati huo huo, Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Musukuma alishauri kabla ya Rais kumpa Mbunge yeyote uwaziri, afanyiwe usaili na vyombo mbalimbali ili kuona kama ana uwezo wa kazi anayopewa kwasababu wengi wanaonekana kuwa na "vyeti vikubwa, lakini uwezo ni mdogo".

Musukuma alisema hata Rais Magufuli wakati anapokea ripoti ya pili ya makanikia alikiri kuwa kuna watu wenye Shahada za Uzamivu (Ph.D), ambao aliwapa kazi kwa kuwaamini kutokana na elimu zao, lakini wamemwangusha.

“Mheshimiwa Mwenyekiti ni vyema tuangalie uwezo wa mtu kichwani badala ya vyeti kwasababu hata ma-Ph.D 17 yaliyoko Benki Kuu ya Tanzania, Mheshimiwa Rais amesema hayajasaidia kitu," alisema Musukuma. 

“Na mimi naona kabisa kwamba kuna watu humu ndani wengine wana vyeti vikubwa, lakini uwezo wa kazi mdogo. 

"Haya yote yanayotokea ni kwasababu kuna watu walipewa kazi wakiwa na vyeti vikubwa, lakini hawakuwa na uwezo wowote.” 

Alisema utaratibu wa kuwapa kazi wasomi kwa kuangalia vyeti vyao ndiyo umeifikisha nchi hapa ilipo kwa kuwa wengi waliokuwa wakipewa kazi serikalini walikuwa na vyeti vya kutisha, lakini hawakuwa na uwezo wa kazi kama alivyosema juzi Ikulu na Rais Magufuli.

“Mheshimiwa Mwenyekiti huu utaratibu wa kuangalia vyeti wakati wa kutoa ajira na hata nafasi za uwaziri umesababisha watu wengi waghushi vyeti ili wapate kazi na kweli wengine wamepata kazi kwa vyeti vya kutisha, lakini uwezo wa kazi hawana na ndiyo hawa hawa wametufikisha hapa.” 

Mbunge wa Ubungo, Said Kubenea, alisema mmoja wa wabunge wa CCM waliotajwa kwenye kashfa ya kusafirisha makinikia nje ya nchi ameshatangaza kwamba hakamatiki.

Alisema mikataba yote ya kifisadi ambayo inaitafuna nchi hivi sasa iliingiwa na serikali ya CCM hivyo vyama vya upinzani havipaswi kusakamwa kwa hasara yoyote ambayo imetokea kwenye sekta ya madini.
Mbunge wa CCM aiomba Serikali iwakamate Chenge na Ngeleja Mbunge wa CCM aiomba Serikali iwakamate Chenge na Ngeleja Reviewed by Zero Degree on 6/16/2017 11:50:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.