Loading...

Serikali haitagawa chakula kwa wananchi wavivu, Samia Suluhu


MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema kamwe Serikali haitagawa chakula kwa wananchi wavivu ambao hawataki kufanya kazi na kusubiri chakula kutoka serikalini. Alitoa kauli hiyo wakati akihutubia mamia ya wananchi wa Manispaa ya Musoma katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Mukendo mjini hapa.

Samia alisisitiza kuwa Serikali itapeleka chakula kwa wananchi ambao mazao yao yaliharibiwa kwa mvua au yalikauka kwa ukame au kwa maafa mengine na sio kwa wananchi wanaokaa vijiweni mchana kutwa bila kufanya kazi wakisubiri neema ya chakula kutoka kwa Serikali.

Aliwahimiza wananchi kote nchini kuendelea kufanya kwa bidii ikiwemo shughuli za kilimo na pindi wanapovuna wajiwekee akiba na waache tabia ya kuuza mazao yote wanayovuna ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa chakula kwenye familia zao.

Pia aliwataka viongozi wa mkoa wa Mara washirikiane na wananchi katika kuwaelemisha mbinu bora za kilimo ili waweze kupata mazao mengi ikilinganishwa na hali ilivyo kwa sasa. Kuhusu tatizo la uvuvi haramu, Samia aliziagiza Kamati za Ulinzi na Usalama kufanya misako ya hali na mali katika kupambana na tatizo hilo ambalo limechangia kupunguza samaki katika maeneo mbalimbali nchini.

Alitoa mfano kwa mkoa wa Mara kuwa ulikuwa na viwanda vinne vya kuchakata samaki, lakini kutokana na shughuli za uvuvi haramu na wa kutumia sumu umepelekea viwanda vitatu kukosa malighafi hiyo na kusitisha uzalishaji.

Samia alisema jambo hilo ni baya kwa sababu limeikosesha Serikali mapato na kusababisha wananchi wakose ajira kutoka kwenye viwanda hivyo jitihada za makusudi lazima zifanyike katika kukomesha uvuvi haramu katika maeneo mbalimbali nchini hasa katika Ziwa Victoria. Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk Charles Mlingwa amewahimiza wananchi wa mkoa wa Mara kuweka itikadi zao kando na washirikiane katika utekelezaji wa miradi.
Serikali haitagawa chakula kwa wananchi wavivu, Samia Suluhu Serikali haitagawa chakula kwa wananchi wavivu, Samia Suluhu Reviewed by Zero Degree on 6/08/2017 12:46:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.