Loading...

Tundu Lissu aibeza ACT Wazalendo


Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amekibeza Chama cha ACT Wazalendo kwa kudai kuwa kuteuliwa kwa viongozi wake katika Serikali ya Rais Dk John Pombe Magufuli ‘JPM’ ni kama kupewa zawadi kwa kazi yao waliyoifanya wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

Viongozi wa ACT Wazalendo
Akizungumza nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar, jana, Lissu alisema ACT ilianzishwa ili kuua upinzani hivyo baada ya kuifanya kazi yao, sasa wanapewa kama zawadi kwa viongozi wake kuteuliwa serikalini.

Akijibu swali kama yeye akiteuliwa atakubali au la, Lissu alisema kwanza hawezi kuteuliwa, lakini pia hata akiteuliwa, hatakubali.

“Kwanza haitatokea rais aniteue kwenye nafasi yoyote na kama akiniteua basi nitamwambia mheshimiwa, mimi napinga mfumo uliokuweka madarakani, nataka katiba mpya, nataka tutengeneze mfumo mpya wenye misingi sawa, ya kuiongoza nchi,” alisema Lissu.

Rais Magufuli alimteua na kumuapisha aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Anna Mghwira, ikiwa ni wiki chache tangu alipofanya uteuzi wa mwanachama mwingine wa chama hicho, Profesa Kitila Mkumbo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Wakati huohuo, ACT-Wazalendo jana ilitangaza kumvua madaraka ya uenyekiti, Anna Mghwira na nafasi hiyo kukaimiwa na Yeremia Maganja.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi zao zilizopo Kijitonyama, Dar, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Samson Mwigamba alisema wanajipongeza kwa rais kuteua viongozi wao kwa vile ni makini, lakini wameamua kumvua uenyekiti Mghwira ili kumpa nafasi nzuri ya kuhudumu ajira yake mpya.

“Hatuwezi kupingana na uteuzi wa rais kwa sababu anajua ACT ina viongozi makini na ndiyo maana amewachagua, lakini kama chama tumeamua kumvua mwenyekiti wetu (Mghwira) na kumkaimisha uenyekiti wa muda, Yeremia Maganja,” alisema Mwigamba.
Tundu Lissu aibeza ACT Wazalendo Tundu Lissu aibeza ACT Wazalendo Reviewed by Zero Degree on 6/08/2017 10:31:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.