Loading...

Hatma waliofutiwa matokeo la 7 hii hapa


SERIKALI imesema watahiniwa 375 waliofutiwa matokeo baada ya kubainika kufanya udanganyifu katika Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) mwaka huu, wanayo njia mbadala ya kuendelea na elimu ya juu yake.

Wanafunzi hao wanaweza kupata elimu ya juu kama watakwenda kujiunga na shule za sekondari za binafsi, watajiunga na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) au watajiunga na vyuo vingine vya wananchi.

Hata hivyo, imesisitiza kuwa wanafunzi hao waliofutiwa matokeo hawatapewa nafasi ya kurudia mitihani hiyo. Juzi Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) lilitangaza kuwafutia matokeo wanafunzi hao kwa mujibu wa kifungu 30 (2) (b) cha Kanuni za Mitihani.

Kwa mujibu wa taarifa ya Habari Leo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha alisema kwamba kwa mujibu wa kanuni za mitihani, watahiniwa hao hawaruhusiwi kurudia mtihani kwani kwa kufanya hivyo ni kuruhusu udanganyifu uendelee.

“Katika makosa makubwa kwenye mitihani hakuna linalozidi udanganyifu kwenye chumba cha mtihani, hivyo watahiniwa waliofutiwa matokeo hawawezi kurudia mtihani na si kwa mwaka huu tu bali hata mwaka mwingine...Sera yetu iliyopo haturudii darasa la saba, hivyo waliofutiwa matokeo ndio kwaheri,” alisema.

Alisema njia mbadala wanayoweza kufanya watahiniwa hao ni kwenda katika shule za sekondari binafsi, vyuo vya Veta au vyuo vya wananchi. “Wanafunzi hawa hawawezi kujiunga na shule za sekondari za serikali kwa kuwa shule zetu ni lazima mwanafunzi awe amefaulu mtihani wa darasa la saba, hivyo kama huna matokeo ya darasa la saba na hujafaulu huwezi kujiunga katika shule za serikali... shule zingine za binafsi hata ukifeli unachukuliwa, hivyo wanaweza kwenda huko,” alisema.

Alifafanua kwamba, wanafunzi waliofutiwa matokeo bado watakuwa na namba zao, kama ambavyo mwanafunzi akipata sifuri bado anakuwa na namba yake. Ole Nasha alifafanua kwamba waliofutiwa matokeo makosa yao yanatokana na udanganyifu katika vyumba vya mitihani lakini wale waliokuwa wamerudia mitihani ilitokana na wizi na uvujaji wa mitihani hivyo makosa hayo ni tofauti.

“Wizi au uvujaji wa mitihani ni kwamba watahiniwa wanaingia kwenye mtihani wakiwa tayari wameshauona mtihani na wanakuwa na majibu lakini udanganyifu katika chumba cha mtihani ni kwamba mtahiniwa anaingia katika chumba cha mtihani na baada ya mtihani kufunguliwa ndipo zinatafutwa mbinu za kupata majibu na hii hutokea kwa mwanafunzi mmoja mmoja hivyo tunawaadhibu tu wale waliohusika,” alisema.

Alisema, “pamoja na kwamba watahiniwa wamefutiwa matokeo lakini mtu yeyote aliyehusika na udanganyifu huu atachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria, ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani na kufukuzwa kazi...Yeyote aliyehusika hatakuwa salama na kwa walimu watafutiwa usajili kwa kuwa hii ni hujuma.”

Alitoa mwito kwa wanafunzi kuzingatia wanayofundishwa darasani na kujiepusha na wizi na udanganyifu kwa kuwa watakapobainika watafutiwa matokeo. Pia aliwataka walimu na wote wanaohusika katika usimamizi kukumbuka na kuzingatia ahadi za taaluma zao kwa kuwa wizi na udanganyifu katika chumba cha mtihani ni makosa makubwa na wakibainika kushiriki hawataachwa salama.

Aliitaka jamii kutoa taarifa pale wanapohisi kuna wizi na uvujaji wa mitihani au udanganyifu ili hatua zichukuliwe kwa haraka kwa kuwa hali hiyo inaharibu mfumo wa elimu nchini. Katika matokeo hayo yaliyotangazwa juzi yakihusisha pia shule zilizorudia mitihani, jumla ya watahiniwa 733,103 kati ya 943,318 ambao kati yao wasichana ni 496,427 na wavulana 446,891 waliotunukiwa matokeo wamefaulu na wamepata alama 100 au zaidi kati ya alama 250.

Idadi hiyo ya watahiniwa waliofaulu ni sawa na asilimia 77.72. Kati yao wasichana ni 382,830 ambao ni sawa na asilimia 77.12 na wavulana ni 350,273 sawa na asilimia 78.38. Mwaka 2017 watahiniwa waliofaulu walikuwa ni asilimia 72.76 hivyo kuna ongezeko la asilimia 4.96.

Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk Charles Msonde alisema hatma ya wanafunzi hao waliofutiwa matokeo, inafahamika wazi kwamba mtahiniwa anapofanya udanganyifu anapaswa kufutiwa matokeo yake kwa mujibu wa kanuni za mitihani hivyo watahiniwa hao wamefutiwa matokeo na walimu wao watachukuliwa hatua na mamlaka zao.

Alisema, “waliofutiwa matokeo hakuna ‘option’ ya kurudia, wewe ulishawahi kuona tukisema waliofutiwa matokeo wanarudia mitihani, hivyo waliofanya udanganyifu ndani ya chumba cha mtihani wanafutiwa matokeo yao”.

Aidha alisema, wakati wa usahihishaji watahini walishangaa kuona kazi za watahiniwa wote wa Shule ya Msingi Mwekako katika Halmashauri ya Chato, mkoani Geita zimeandikwa kwenye karatasi tofauti na zilizotolewa na NECTA na majibu yao yalikuwa na mfanano wa kupata na kukosa usiokuwa wa kawaida.

Dk Msonde alisema watahiniwa walipohojiwa walikiri kuwa majibu walikuwa wakipewa nna Mwalimu Mkuu, Habibu Rweshabura ambapo pia walishirikiana na wasimamizi Salvatory Stanslaus, Misana Kujerwa, Gwambala Shadrack na mlinzi MG 147844 Nelson Ntarambe.

Aidha alisema katika Shule ya Msingi Bariadi Alliance, Mkoa wa Simiyu walimu Simon Shepard, Ogwang Andrew na Thomas Malongo walifanya kikao maalum cha kuweka mikakati ya kufanya udanganyifu wakati mitihani ilipokuwa ikifanyika.

“Walimu hawa walipanga kula njama na wasimamzi wa mitihani kutoa karatasi ya maswali nje ya chumba cha mtihani baada ya kufungua mtihani, walimu kukokotoa majibu na kuyaandika kwenye rula tano ambazo walipewa watahiniwa watano ili wafikishe majibu hayo pia kwa baadhi nya wanafunzi waliokuwa wamepangwa kuoneshwa,” alisema.

Alisema wakati wa utekelezaji ofisa ufuatiliaji alizikamata rula hizo na katika mahojiano watahiniwa walikiri kosa na kufichua mpango mzima kama ulivyofafanuliwa ambapo pia wahusika wengine wa udanganyifu huo ni Grace Kipondya na Grayson Ngalla.

Pia alisema, wakati mtihani wa somo la Sayansi ukiendelea kufanyika msimamizi Faustine Mtesigwa aliwakamata watahiniwa wawili wakiwa na karatasi zenye majibu katika Shule ya Msingi Msufini, iliyopo Halmashauri ya Geita Vijijini.

Alisema uchunguzi zaidi uliofanyika katika watahiniwa wa shule hiyo ulibaini mfanano usio wa kawaida wa majibu ya kupata na kukosa kwenye somo la Kiingereza na Hisabati. “Katika somo la Hisabati baadhi ya watahiniwa walikosa swali la 41 kwa kuandika jibu +27 badala ya -27.

Imebainika watahiniwa wote walikosea jibu kutokana na aliyewaonesha kukosea kunakili swali kwa kuweka -6 badala ya +6 iliyokuwa kwenye swali. Alisema mfanano huo unaonesha kuwa, uongozi wa shule ulishirikiana na baadhi ya wasimamizi kufanikisha udanganyifu huo ambapo aliwataja wahusika kuwa ni Mwalimu Mkuu wa Shule, Venance Muhogo, Msimamizi Neema Severine na Marima Tanganyika.
Hatma waliofutiwa matokeo la 7 hii hapa Hatma waliofutiwa matokeo la 7 hii hapa Reviewed by Zero Degree on 10/25/2018 05:35:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.