Loading...

Drogba atangaza rasmi kustaafu kucheza soka


Mchezaji nyota kutoka Ivory Coast aliyeng'ara na klabu ya Chelsea ya Uingereza, Didier Drogba, amethibitisha kustaafu kucheza mpira,"baada ya miaka 20".

Mshambuliaji huyo mwenye miaka 40 aliichezea Chelsea mara mbili tofauti na kufunga jumla ya magoli 164 katika mechi 381. Pia amehinda mataji manne ya ligi kuu ya England na taji la klabu bingwa Ulaya mwaka 2012.

Amemalizia miezi 18 ya maisha yake ya soka nchini Marekani katika klabu ya Phoenix Rising, ambayo yeye ni mmiliki mwenza.

"Baada ya miaka 20, nimeamua kustaafu kucheza mpira," ameiambia BBC.

Ilitarajiwa gwiji huyo wa mpira kustaafu baada ya mechi ya fainali ya ligi ya Marekani mapema mwezi huu ambapo timu yake ilifungwa goli 1 bila majibu na klabu ya Louiville City.

"Ni njia bora zaidi ya kumaliza safari yangu kwa kusaidia vipaji vipya kunyanyuka na kung'ara," amesema.

Drogba alisubiri mpaka alipofikisha miaka 23 kuanza kucheza mpira kwenye ngazi ya ushindani wa juu aliposajiliwa na Guingamp kutoka klabu ya daraja la pili ya Le Mans mnamo Januari 2002.

Alihamia klabu ya Marseille miezi 18 baadae na baada ya mwaka mmoja akatua Chelsea kwa dau la pauni milioni 24, hiyo ilikuwa mwaka 2004. Nyota yake iling'ara zaidi na miamba hiyo ya London.

Drogba alishinda mataji matatu ya Ligi ya England ndani ya misimu yake nane ya awali na Chelsea, ikiwemo misimu yake miwili ya mwanzo na klabu hiyo. Pia alishinda makombe manne ya FA na mawili ya ligi.

Pia alishinda kiatu cha dhahabu kwa kufunga magoli zaidi kwa misimu ya 2007-07 na 2009-10.

Aliondoka Chelsea mwaka 2012 kwa heshima kubwa baada ya kufunga penalti ya ushindi kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich.

Kutoka Chelsea Drogba alielekea Uchina kwa miezi sita na kukipiga na klabu ya Shanghai Shenhua na baadae Uturuki kwa mwaka mmoja unusu na klabu ya Galatasaray.


Alirudi tena Chelsea katika msimu wa 2014-15, ambapo alifunga mabao saba. Alishinda taji lake la nne la Ligi ya England na Kombe la Ligi kwa mara ya tatu.

Drogba ni mchezaji wa nne kwa kufunga magoli mengi zaidi kwenye historia ya Chelsea.

Mwaka 2015, alienda Marekani na kuchezea klabu ya Montreal Impact na baadae kuwa mchezaji na mmiliki wa Phoenix Rising.

Amelifunia taifa lake magoli 65 katika mechi 105, amecheza makombe ya dunia matatu na kuutuzwa kama mchezaji bora wa mwaka wa Afrika mara mbili.

Mpatanishi wa amani

Mara baada ya kuliwezesha taifa lake kufuzu kwa kombe la dunia mwaka 2005, Drogba aituma ujumbe wa amani kwa taifa lake ambalo lilikuwa kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe. Baada ya wiki moja mapambano yalizimwa.

"Kabla ya kuwa mchezaji, mimi ni binadamu, mwanaume. Nina maisha yangu, ninataka kuishi kwenye nchi yenye amani. Nchi yangu ilikuwa kwenye lindi la vita na fadhaa. Nchi imegawanyika na kitu pekee kinachotuunganisha ni mpira" alisema hayo mwaka 2005.

"Nilipoamua kuchezea Ivory Coast sikujua kwamba ipo siku ningelikuwa nahodha na kuliongoza taifa kwenye kombe la dunia. Sikuwahi kufikiria kuwa ningefanya kitu cha kukumbukwa kwenye historia ya nchi yangu. Nilipata pia fursa ya kuichezea Ufaransa, lakini mafanikio niliyoyapata na Ivory Coast- na kama mwanadamu- sidhani kama ningeyafikia kwa kuchezea Ufaransa."
Drogba atangaza rasmi kustaafu kucheza soka Drogba atangaza rasmi kustaafu kucheza soka Reviewed by Zero Degree on 11/22/2018 08:35:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.