Majaji 5 kutoka China watembelea Mahakama ya Tanzania
Msajili Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Katarina Revocati akiwa katika mazungumzo pamoja na Majaji kutoka Mahakama Kuu Zhejiang iliyopo Jamhuri ya Watu wa China. |
Majaji hao kutoka jimbo la Zhejiang la nchini China pia wameitembelea Mahakama ya Tanzania kwa lengo la kujifunza zaidi na kubadilishana uzoefu hasa kuhusu adhabu zinazotolewa na Mahakama kwa ajili ya kuirekebisha jamii.
Akizungumza na Majaji hao, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Katarina Revocati amewaambia kuwa Mahakama ya Tanzania ni chombo huru kinachotekeleza majukumu yake kwa uhuru pasipo kuingiliwa na Mihimili mingine.
Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Katarina Revocati (kushoto) akimpatia zawaji mmoja wa Majaji kutoka Mahakama Kuu Zhejiang nchini China. |
Akizungumzia adhabu zinazotolewa na Mahakama katika kuirekebisha jamii hasa zile za kifungo cha nje, Msajili Mkuu alisema adhabu hizo hutolewa kwa mujibu wa sheria na kwa vigezo mbalimbali ikiwemo kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani na kufanya shughuli za uzalishaji ili kuisaidia jamii.
Alisema Mahakama ya Tanzania imekuwa ikishauri matumizi ya adhabu mbadala ikiwemo kazi za nje badala ya adhabu za kifungo gerezani. Kupitia adhabu hizi, wafungwa watatumika pia kufanya kazi za uzalishaji mali na kuisaidia jamii.
Kwa upande wao, Majaji hao kutoka nchini China wamesema wamefika nchini kujifunza mfumo wa utoaji haki unavyofanya kazi na hasa kuhusu adhabu zinazotolewa na Mahakama katika kuirekebisha jamii kwa kuwa mfumo huo pia hutumiwa na Mahakama zao.
Kwa mujibu wa Majaji hao, China inazo fursa nyingi za kuwaendeleza wanasheria kitaaluma na hivyo wametoa wito kwa Mahakama ya Tanzania kutumia fursa hizo katika kuwaendeleza watumishi wake kama ambavyo nchi nyingine zimekuwa zikifanya.
Majaji 5 kutoka China watembelea Mahakama ya Tanzania
Reviewed by Zero Degree
on
11/16/2018 06:20:00 PM
Rating: