Loading...

Odinga agoma kuachana na siasa


KIONGOZI wa upinzani chini hapa, Raila Odinga, amesema hana mpango wa kuachana na siasa hivi karibuni licha ya kukabidhiwa wadhifa mkubwa katika Umoja wa Nchi za Afrika (AU).

Odinga aliyasema hayo juzi akiwa wilayani Yimbo na akawataka wanamtaka kuachana na siasa baada ya kupata uteuzi huo kutopoteza muda wao na badala yake watafute kazi nyingine ya kufanya.

“Ningependa kufafanua kwamba uteuzo wangu wa hivi karibuni hautaathiri shughuli zangu za siasa,” Odinga aliwaambia waombolezaji wakati wa mazishi ya William Odhiambo Okello.

“Hivyo nashauri kuachwa mjadala juu ya hatma yangu katika siasa,”aliongeza kiongozi huyo mkuu wa upinzani.

Mwanzoni mwa mwezi huu, Odinga alichaguliwa kuwa Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Afrika kuhusu miundombinu wadhifa ambao ni mkubwa kidiplomasia katika Umoja huo.

Uteuzi huo ndiyo uliwasukuma wabunge wengi kutoka Mkoa wa Mlima Kenya kumtaka kiongozi huyo kuachana na siasa za nchini hapa.

Uteuzi huo pia umekuja wakati nchi hii imeshaanza mjadala nani atakuwa mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta kutoka upande wa vyama vya upinzani na chama tawala cha Jubilee.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, kambi ya Makamu wa Rais William Ruto inaeleza kwamba uteuzi huo unaweza kumzuia Raila kuingia tena katika mbio za kuwania kiti cha urais na hivyo mwaka 2022 kumnufaisha Ruto.

Hali hiyo pia inaripotiwa kuwaacha njia panda washirika na wafuasi wake ambao wamekuwa wakikuna vichwa wakihoji kama nafasi hiyo itamruhusu aendelee na shughuli za siasa, jambo ambalo aliamua kuliweka wazi.

“Hata kama nitakuwa nikizunguka kwenye miji mkuu yote ya nchi za Afrika ngome yangu kuu itakuwa ni Nairobi. Sitakwenda mahali popote,”alifafanua kiongozi huyo.

“Nafikiri wale wote wanaodhani nitaachana na siasa wanaota ndoto za mchana,”aliongeza Odinga.

Alisema viongozi wa Chama Cha NASA walishajitolea mengi katika ukombozi wa taifa hili na hivyo wanapaswa kuyaendeleza.
Odinga agoma kuachana na siasa Odinga agoma kuachana na siasa Reviewed by Zero Degree on 11/05/2018 10:05:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.