Miss Tanzania atikisa China
MWAKILISHI wa Tanzania kwenye mashindano ya urembo ya Dunia Queen Elizabeth Makune ameingia 15 bora ya warembo wanaopewa nafasi ya kushinda taji la ulimbwende kwa mwaka huu.
Shindano hilo la 68 la dunia limepangwa kufanyika Desemba nane jijini Sanya, China.
Katika taarifa ya mtandao wa GoPageant ambao huelezea na kuchambua mashindano mbalimbali ya urembo duniani, ulimtaja Queen Elizabeth ni mmoja wa warembo 15 kati ya 113 wanaoshiriki shindano hilo wanaopewa nafasi kubwa ya kutwaa taji hilo lenye heshima duniani katika masuala ya urembo.
Mwandaaji wa Miss Tanzania, Basila Mwanukuzi ameomba watanzania kuendelea kumpigia kura kwa wingi mshiriki huyo ili aweze kuipeperusha vema bendera ya Tanzania katika mashindano hayo makubwa ya urembo duniani.
Basila ambaye ni Miss Tanzania mwaka 1998, aliwataka watanzania kumpigia kura mrembo huyo kupitia tovuti ya Miss World ya www.missworld.com.
Warembo wengine wanaopewa nafasi kubwa ya kutwaa taji hilo ni Shrinkhala Khatiwada (Neval), Dayana Martinez (Puerto Rico) na Annukreethy Vas kutoka India.
Wengine ni Miss Chile, Anahi Hormazabal ambaye kama atashinda basi hii itakuwa ni mara ya pili kwa nchi hiyo kuondoka na taji hilo, Andrea Szarvas (Hungary), Maeva Coucke (Ufaransa), Agata Biernat (Poland), Morgane Theresine (Guadalupe), Solaris Barba (Panama), Elya Nurshabrina (Indonesia).
Pia yupo Taylah Cannon kutoka nchini Australia, Vanessa Ponce (Mexico) na Natalya Stroeva (Urusi).
Miss Tanzania atikisa China
Reviewed by Zero Degree
on
12/04/2018 06:50:00 PM
Rating: