Yanga yashusha kifaa kipya
YANGA ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa winga wa Singida United, Tibar John katika kukiimarisha kikosi chao wakati dirisha la usajili wa dirisha dogo likikaribia kufungwa. Usajili wa dirisha dogo tayari umefunguliwa tangu Novemba 15 ambao utafungwa Disemba 15, mwaka huu.
Yanga, tayari ipo kwenye mazungumzo ya mwisho kwa ajili ya kukamilisha usajili wa beki wa Lipuli, Ally Mtoni, Eliud Ambokile (Mbeya City), Vitalis Mayanga (Ndanda FC), Kenny Ally (Singida United) na winga kutoka DR Kongo, Reuben Bomba ambaye tayari yupo nchini. Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, Yanga inataka kumsajili winga huyo katika kukiimarisha kikosi chake katika kuelekea mzunguko wa pili wa ligi.
“Wakati wowote Tibar atasaini mkataba wa kuichezea Yanga katika usajili huu wa dirisha dogo, ni baada ya viongozi kuanza kufanya naye mazungumzo na yeye mwenyewe kuonyesha nia ya kuja kuichezea Yanga.
“Na kilichokuwa kinachelewesha Tibar asisaini mkataba ni mechi ya ligi ya Tanzania Prisons ambayo viongozi wa Yanga walikuwa kwenye maandalizi ya mchezo huo na kusababisha kusitisha baadhi ya vitu likiwemo hilo la usajili.
“Hivyo, baada ya mechi hiyo na Prisons, basi viongozi watakuwa katika nafasi nzuri ya kukamilisha usajili huo wa winga huyo mwenye kasi ndani ya uwanja,” alisema mtoa taarifa huyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili na Mashindano wa Yanga, Hussein Nyika aliliambia gazeti hili kuwa: “Wiki hii ndiyo tunaanza usajili rasmi wa wachezaji wapya katika usajili wa dirisha dogo, hivyo ni vigumu kumtaja moja kwa moja Tibar, tusubirie muda ukifika tutaweka wazi.”
Yanga yashusha kifaa kipya
Reviewed by Zero Degree
on
12/07/2018 05:35:00 PM
Rating: