Loading...

Mapokezi ya Ruge yaisimamisha Dar

Umati wa wananchi, waombolezaji, ndugu, jamaa na marafiki, wakilisindikiza gari lililobeba jeneza lenye mwili wa marehemu Ruge Mutahaba, baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam jana, ukitokea nchini Afrika Kusini. PICHA: MIRAJI MSALA

WAKAZI wa Dar es Salaam jana walilazimika kusitisha shughuli zao kwa muda kupisha mapokezi ya mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi wa Clouds Media Group (CMG), Ruge Mutahaba.

Mwili huo unaotarajiwa kuzikwa keshokutwa wilayani Bukoba mkoani Kagera, uliwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa tisa alasiri ukitoka Afrika Kusini. 

Maelfu ya waombolezaji walijipanga vituo vyote 11 vilivyopangwa mwili huo kupita hadi kwenye Hospitali ya Lugalo, jijini ulikohifadhiwa.

Mapokezi hayo yaliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na hadi mwili huo ulipohifadhiwa kwenye hospitali hiyo ya jeshi, msafara ukichukua takribani saa tatu tangu kuwasili kwa mwili huo uwanja wa ndege.

Mara baada ya kuwasili uwanjani huko, mwili huo uliingizwa kwenye gari maalum la kubeba maiti lenye namba za usajili T 195 DGZ na msafara ulianza kwenda Hospitali ya Jeshi Lugalo saa 10:00 jioni.

Ruge (48), alifariki dunia Jumanne Afrika Kusini ambako tangu mwishoni mwa mwaka jana, alikuwa anapatiwa matibabu ya kibingwa kutokana na maradhi ya figo.

Safari ya kwenda Lugalo ilishuhudiwa na Watanzania kupitia matangazo ya moja kwa moja yaliyorushwa na vituo vya luninga vya ITV na Clouds TV na mitandao mingine.

Baadhi ya waombolezaji walianguka na kuzirai wakati wa msafara huo kwa kile kilichonekana kukosa hewa kutokana na msongamano mkubwa wa watu uliokuwapo kila kituo kilichokuwa kimepangwa.

Msafara huo ulipita katika vituo 11 vilivyotajwa awali ambavyo ni Barabara ya Nyerere, Buguruni, Karume, Magomeni, Hoteli ya Morocco, Sinza Kijiweni, Bamaga, ITV, Clouds, Kawe na Hospitali ya Lugalo.

Msafara ulipofika eneo la Magomeni, ulilazimika kusimama kwa muda na Mkuu wa Mkoa (Makonda) akalazimika kushuka ili kutoa maelekezo kutokana na waendesha pikipiki kuzingira gari lililokuwa na mwili na kusababisha msafara kutokwenda ilivyopangwa.

Idadi ya waombolezaji iliongezeka zaidi msafara huo ulipofika Tandale na kuwa na msongamano mkubwa wa magari hadi kwenye maeneo ya Sinza.

Vijana waliokuwa wakiusindikiza mwili huo kwa kukimbia, walikuwa wanaimba huku wengine wakitumia nguo zao kufuta gari lililobeba mwili huo.

Pia, baadhi ya wananchi walijitokeza pembezoni mwa barabara hizo wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe wa kumpa heshima Ruge.

MWILI WAWASILI CLOUDS


Majonzi na vilio vilitanda baada ya mwili wa Ruge kuwasili kwenye ofisi za Clouds zilizoko Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Wafanyakazi, wasanii na viongozi mbalimbali waliokuwa ndani ya ofisi hizo, walipata nafasi ya kusali pamoja baada ya jeneza lake kutolewa ndani ya gari na kuingizwa ndani ya ofisi hizo.

Saa 12.48 jioni, mwili huo uliondolewa kwenye ofisi hizo na kupelekwa Hospitali ya Jeshi Lugalo.

GWAJIMA, BABU SEYA


Akiwa nyumbani kwa baba wa marehemu Mikocheni jijini Dar es Salaam jana mchana, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, aliwaambia waombelezaji Ruge ameondoka kabla nguvu kazi yake haijatumika vizuri.

Alisema kwa maneno machache anaweza kueleza kuwa taa ya Clouds Media imezimika katikati ya giza, hivyo chombo hicho cha habari kinapaswa kujipanga namna ya kutoka gizani.

"Sababu za kufa zipo nyingi, unaweza kufa kwa sababu umri umefika, yaani ametumika sasa anaenda kupumzika. Sababu ya pili ni kukatizwa na watu, najua wapo ambao wanataka kukataa kuwa mtu hawezi kukatizwa uhai, mfano ni Yesu alikatizwa uhai wake na watu. Sababu ya tatu ni ugonjwa, mtu anaugua na kufa," Gwajima alisema.

Alisema kuwa katika maisha, kuna marafiki wazuri wa maisha na wabaya, hivyo marafiki wabaya hawawezi kukuzungumzia yale mazuri uliyoyafanya.

"Duniani kuna falsafa unapokuwa mtu mzima, unatengeneza marafiki wengi na maadui wengi na adui siku zote hawezi kukuzungumzia vizuri, lakini la muhimu kwa sasa, Ruge alikuwa ni kijana mzuri, alikuwa anapenda watu na amewainua wengi. Watu wengi wanalia kwa sababu amewagusa maisha yao, lakini adui wa maisha yupo na rafiki wa maisha yupo," alisema.

Gwajima alisema Ruge alikuwa akizungumza naye mambo mengi ya ndani, lakini kwa sasa hawezi kuyasema kwa kuwa hayupo tena duniani.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, alisema Ruge amegusa mioyo ya watu kwa kuwa siku zote alikuwa anawafungulia njia na kuwaonyesha fursa zilizopo.

"Mimi amenisaidia sana na aliahidi atanisaidia kwa kuwa alinieleza dhamira yake ni kuwaendeleza vijana, nenda Ruge Mungu atakulipa fungu lako," alisema.

Msanii Nguza Viking 'Babu Seya' alisema: "Ruge alikuwa mwanangu na katika mateso ya kifungo changu, alikuwa ni shahidi na siwezi kusema mengi.

Mbunge wa Jimbo la Mikumi, Joseph Haule 'Profesa Jay' (Chadema), alisema Ruge alikuwa ni mtu wa watu na alikuwa "kocha na mwenye maono ya kipekee".

Chanzo: Nipashe
Mapokezi ya Ruge yaisimamisha Dar Mapokezi ya Ruge yaisimamisha Dar Reviewed by Zero Degree on 3/02/2019 09:35:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.