Loading...

Sumaye afunguka kumfuata Lowassa


WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amesema hana mpango wa kumfuata Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyeamua kurejea Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Machi Mosi, Lowassa (65), aliyekuwa mgombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2015 kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alirejea CCM na kupokewa na viongozi wakuu wa chama hicho waliongozwa na Mwenyekiti, Dk. John Magufuli kwenye ofisi ndogo za Lumumba jijini Dar es Salaam.

Katika mahojiano na Nipashe mwishoni mwa wiki kuhusu uamuzi huo wa Lowassa na kama naye yuko mbioni kurejea chama tawala, Sumaye alisema kuwa yeye bado ni mwanachama na mfuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Sumaye ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, alisema Lowassa kurejea CCM ni uhuru wake na uamuzi wake, na kama hajashinikizwa na mtu, haoni tatizo lolote kurudi kwake kwenye chama chao cha zamani.

"Mimi ni Chadema. Kuhama chama ni uhuru wa mtu na sioni tatizo lolote Lowassa kuhama chama. Ni maamuzi yake kurudi CCM, maana alihama CCM akaja Chadema, mbona halikuwa tatizo na kwanini kurudi CCM liwe tatizo?" Sumaye alihoji.

Kuhusu madai kwamba wana mpango wa kumrejesha Sumaye CCM, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, alidai chama hicho hakina utaratibu wa kufuata watu na kuwaomba kujiunga nacho, bali wao wenyewe hukifuata baada ya kuridhishwa na utendaji wake.

"Hatuna mipango ya kufuata watu, hilo ndiyo jibu langu," Polepole alisema.

Agosti 22, 2015, Sumaye (69), alitangaza kuihama CCM na kujiunga na Chadema, hivyo kuwa Waziri Mkuu mstaafu wa pili kujiondoa chama tawala katika historia ya Tanzania, baada ya Lowassa kufanya hivyo Julai 28, 2015.

Sumaye ambaye alidumu nafasi ya Waziri Mkuu kwa miaka yote 10 ya utawala wa awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa, alitaja sababu za uamuzi wake wa kujiondoa CCM kuwa ni kukithiri kwa rushwa ndani ya chama hicho tawala.

Wakati wa kurejea CCM, Lowassa alitamka maneno machache baada ya salamu za chama akisema: "Nimerudi nyumbani".

Lowassa aliweka rekodi ya kuwa Waziri Mkuu wa kwanza kuhamia upinzani katika historia ya siasa za Tanzania, baada ya jina lake kushindwa kupenya katika majina matano yaliyoteuliwa na Kamati ya Maadili ya chama hicho, kuwania urais kupitia CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015.

Katika uchaguzi huo, Lowassa aligombea Ukawa, iliyoundwa na Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na NLD na kupata kura 6,072,848 (asilimia 39.97) akiwa nyuma ya Dk. Magufuli aliyetangazwa mshindi kwa kura 8,882,935 (asilimia 58.46).

Wakati akitangaza kuihama CCM Julai 28, 2015, Lowassa alisema: "Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, Kamati ya Maadili iliyokata jina langu na majina mengine, haina madaraka ya kuchuja na kupendekeza majina miongoni mwa wale wanaoomba kugombea urais kupitia CCM, lakini ilifanya hivyo."

Katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Monduli juzi, Edward Lowassa, alimshukuru Rais Magufuli kwa moyo wake wa upendo na ushawishi alioutumia kumrejesha CCM. "Ninamshukuru Rais Magufuli kwa moyo wake wa upendo na ushawishi wake wa hali ya juu alioutumia mpaka mimi kuja kwenye Chama Cha Mapinduzi, alifanya kazi kubwa sana, namheshimu sana, namshukuru sana," Lowassa alisema.
Sumaye afunguka kumfuata Lowassa Sumaye afunguka kumfuata Lowassa Reviewed by Zero Degree on 3/11/2019 07:50:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.