Loading...

Alichokisema Nyalandu baada ya kuachiwa kwa dhamana


Aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu amesimulia namna alivyokamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kuhojiwa kwa saa kadhaa kabla ya kuachiwa kwa dhamana leo mchana Mei 28, 2019 na kutakiwa kuripoti polisi kesho.

Waziri huyo wa zamani wa Maliasili na Utalii ambaye kwa sasa ni mwanachama wa Chadema alikamatwa jana na maofisa wa Takukuru katika kata ya Itaja Singida Kaskazini.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda Polisi Mkoa wa Singida, Sweetbert Njewike amesema, “Sisi hatukuwa na shida yoyote na watuhumiwa, Takukuru waliomba nafasi ya kuwahifadhi watuhumiwa kwa hivyo jukumu letu lilikuwa ni kuwahifadhi tu.”

Akizungumza na Mwananchi leo, Nyalandu amesema alikamatwa jana saa 8 mchana akiwa kwenye kikao cha ndani na vijana 29 katika kijiji cha Itaja jimbo la Singida Kaskazini.

Amesema walivamiwa na watu walioanza kuuliza alipo Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Singida, Shaban Lyimo ambaye alisimama na kuwaeleza watu hao kuwa walikuwa katika kikao cha ndani cha Chadema.

“Kwanza walituliza kibali (cha kikao), Lyimo akawajibu kuwa hatuna na ni kikao cha ndani hakihitaji kibali. Wakasema kuwa wao wametoka Takukuru Mkoa wanawahitaji watu wakaninyooshea kidole mimi (Nyalandu) na David Jumbe pamoja na mwenyekiti (Lyimo),” amesema Nyalandu.

Chanzo: Mwananchi
Alichokisema Nyalandu baada ya kuachiwa kwa dhamana Alichokisema Nyalandu baada ya kuachiwa kwa dhamana Reviewed by Zero Degree on 5/28/2019 05:40:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.