Loading...

Serikali yapigilia nyundo ukomo wa urais

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi

SERIKALI imesisitiza kuwa muda wa Rais kuwa madarakani ni vipindi viwili tu na kusisitiza kuwa hakuna mtu yeyote anayeweza kubadili utaratibu huo uliopo kwa mujibu wa katiba.

Hata wakati wa uhai wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alisema enzi za utawala wake alisisitiza kuwa masuala ya ukomo wa urais ni vipindi viwili licha ya nchi kuwa katika mfumo wa chama kimoja wakati huo. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua Kongamano la Kumbukizi ya Mwalimu Julius Nyerere lililoandaliwa na Kigoda cha Mwalimu Nyerere katika taaluma za umajumui wa Afrika kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi.

"Mwalimu alisisitiza masuala ya ukomo wa urais ni vipindi viwili tu licha ya nchi kuwa katika mfumo wa chama kimoja. Nasema hakuna wa kulibadili hili, tutaendelea kuwa na vipindi viwili vya urais," alisema Prof. Kabudi.

“Tusihusishe kesi iliyoko mahakamani na rais aliyepo. Huyo (aliyefungua kesi) ni raia na ana haki ya kwenda mahakamani. Mwalimu Nyerere alisisitiza ukomo wa vipindi viwili vya urais na wako waliojaribu kutaka kulibadili hilo, lakini aliwashukia kama mwewe kwa sababu aliamini hili ni moja ya misingi ya taifa," aliongeza.

Naye Mgoda wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Prof. Rwekaza Mukandala, alisema mchango wa Mwalimu Nyerere katika ujenzi wa taifa la Tanzania hautasahaulika.

Alisema mwaka 1993, Mwalimu Nyerere alisambaratisha juhudi za wabunge waliotaka kuuvunja Muungano na kutaka muundo wa serikali tatu, pamoja na kuondoa ukomo wa muda wa rais madarakani.

"Mwalimu Nyerere aliamini na kusimamia kwenye fikra na misimamo, misingi ya ubinaadamu na alisimamia katika maandiko ambayo hadi leo viongozi wengi wa Bara la Afrika wanayafuata," alisema.

Prof. Mukandala alisema Mwalimu Nyerere alilipa kipaumbele suala la uongozi kwa kuanzisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mwaka 1961 alifungua majengo ya chuo hicho na wiki moja baadaye alifungua chuo cha Kivukoni, na Chuo cha Polisi.

"Mwalimu alisema kiongozi lazima awe na sifa kuu tatu. Kwanza awe na uwezo wa kufikiri, pili awe na uwezo wa kujieleza kwa ufasaha, tatu awe mwenye kumudu vizuri kazi yake," alisema Prof. Mukandala.

"Mwalimu Nyerere alikemea mbwembwe, misafara mirefu ya magari ya viongozi, alichukia mishahara mikubwa, viongozi kuwa mabepari. Hakupenda vyeti kutundikwa ukutani, alikemea majina ya vyeo bali alipenda tuitane ndugu."

Prof. Mukandala alisema Mwalimu Nyerere mwaka 1995 alitoa mchango mkubwa wa kupatikana kwa mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Naye Makamu Mkuu wa UDSM, Prof. William Anangisye, alisema Oktoba 25, mwaka huu, UDSM itatimiza miaka 58 tangu ilipoanzishwa.

Alisema kuanzia mwaka 1970 Mwalimu Julius Nyerere ndiye alikuwa Mkuu wa Kwanza wa UDSM hadi alipong'atuka mwaka 1985.

Chanzo: Nipashe
Serikali yapigilia nyundo ukomo wa urais Serikali yapigilia nyundo ukomo wa urais Reviewed by Zero Degree on 10/11/2019 08:20:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.