Loading...

Watalii 1,000 Israel kutua nchini

Mwenyekiti wa Bodi ya TTB, Jaji mstaafu Thomas Mihayo

ZAIDI ya watalii 1,000 kutoka Israeli wanatarajia kuwasili nchini mwezi huu kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na Zanziba kwa ajili ya shughuli za kitalii.

Watalii hao wanatarajiwa kuwasilia katika makundi matatu kuanzia leo, wengine Octoba 12 na 13, mwaka huu. 

Hii ni mara ya pili kwa watalii kwa idadi hiyo kutoka nchini humo, baada ya Aprili mwaka huu kuwasili kupitia KIA kwa ndege tatu tofauti.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya TTB, Jaji mstaafu Thomas Mihayo, alisema watalii hao wanatarajia kutembelea Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Hifadhi za Taifa za Serengeti, Tarangile na Zanzibar.

"Sekta ya utalii Tanzania imefunguka rasmi. Tunaona idadi kubwa ya watalii wameanza kuelewa vivutio tulivyo navyo na wameanza kumiminika. Oktoba ni mwezi wa neema sana kwetu kwa sababu unakuwa na idadi kubwa ya wataalii," alisema Jaji Mihayo.

"Tunaamini kwamba hata amani tuliyo nayo Tanzania inachangia watalii kuongezeka. Bila hivyo sidhani kama wangemiminika hivi hata kama tungekuwa na vivutio vizuri namna gani,” aliongeza.

Mwenyekiti huyo alisema ni wakati mwafaka pia kwa Watanzania hususani katika maeneo ambayo yanatembelewa na watalii hao kuchangamkia fursa za kibiashara.

"Unajua Tanzania ndiyo kwanza soko linafunguka. TTB tumefanya kazi kubwa ya kutembea katika nchi mbalimbali kutangaza vivutio tulivyo navyo na sasa tunaona dunia imeanza kuvielewa," alisema na kuongeza:

"Ni wakati na sisi Watanzania kuchangamkia fursa mbalimbali, tuhakikishe wanapokuja wanatuachia pesa nyingi kwa hiyo tutengeneze bidhaa ambazo wakiziona lazima wanunue na fursa nyinginezo za kibiashara."

Chanzo: Nipashe
Watalii 1,000 Israel kutua nchini Watalii 1,000 Israel kutua nchini Reviewed by Zero Degree on 10/05/2019 07:35:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.