Loading...

Sababu kuu zilizoifanya Tanzania kufikia uchumi wa kipato cha kati

Msemaji wa serikali, Dokta Hassan Abasi

Serikali ya Tanzania imesema utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati iliyobuni ajira kwa Watanzania wengi ni kati ya vitu ambavyo viliivutia Benki ya dunia kuitangaza nchi hiyo kama taifa lenye kipato cha kati.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma Msemaji wa serikali, Dokta Hassan Abasi amesema Kwamba takwimu za kipato cha waliopata ajira ndio sehemu kubwa iliyochukuliwa na Benki ya dunia kuthibitisha kwamba pato la Watanzania limeongezeka.

Afisa huyo wa serikali alitaja ujenzi wa mradi wa umeme wa Rufiji wa megawati 2500 kama mojawapo ya mambo yaliyosababisha kuimarika kwa uchumi wa taifa hilo.

Bwana Abbas amesema kwamba mradi huo umebuni zaidi ya ajira 3500.

''Katika miaka 59 tunayoelekea ya Uhuru na katika miaka mitano ya uongozi wa rais Magufuli kama kuna eneo tumewekeza kwa kiasi kikubwa na limesaidia sana kuchemsha uchumi ni katika ujenzi ambao wengine wanaita maendeleo ya vitu. Kwa mfano unapozungumzia mradi wa umeme wa Rufiji umebuni ajira ya zaidi ya 3500'', alisema afisa huyo wa serikali.

Mbali na uongozi thabiti wa rais Magufuli katika kudhibiti matumizi ya fedha na kukabiliana na ufujaji wake, Bwana Abbas amesema kwamba taifa la Tanzania limeimarika kiviwanda hali ya kwamba lina karibia viwanda 60 tangu lilipojipatia Uhuru, huku uongozi wa rais Magufuli ukifanikiwa kuanzisha zaidi ya viwanda elfu nane katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake.

''Hivi sasa kwa mfano tuna uwezo wa kuunganisha matinga humu nchini, kuunganisha mabasi kuzalisha nondo ,mabati na kadhalika'', aliongezea.

Benki ya dunia siku ya Jumatano iliiorodhesha Tanzania katika orodha ya nchi za uchumi wa kipato cha kati.

Hatua hiyo inajiri miaka mitano kabla ya ruwaza ya maendeleo ya taifa hilo ambapo ilikuwa imelenga kuafikia kiwango hicho kufikia 2025.

Na kufuatia hatua hiyo rais wa Tanzania John Pombe Magufuli aliwapongeza wananchi wa taifa hillo kwa mafanikio hayo.

Katika wiki yake ya kwanza madarakani mnamo mwezi Novemba mwaka 2015 , rais Magufuli aliwashangaza wengi alipositisha ziara za maafisa wa serikali kwenda ngambo mara kwa mara.

Hatua hiyo ilipokelewa vyema na Watanzania kuwa maafisa wa serikali walionekana kama wanaofuja fedha za umma kwa kufanya ziara za mara kwa mara ughaibuni, ziara nyingi zikiwa hazina manufaa yoyote kwa Watanzania.

Ni nadra kwa rais Magufuli kufanya ziara katika nchi za kigeni na maafisa hulazimika kupata vibali vya kusafiri kutoka idara zinazochunguzwa kwa ukaribu na ofisi yake.

Ripoti ya Benki kuu nchini Tanzania mapema mwaka 2017 ilifichua kwamba serikali iliokoa takriban $430m (£330m) kwa kupunguza safari za ughaibuni kati ya mwezi Novemba 2015 hadi Novemba 2016.

Je ni vigezo gani vinavyotumiwa na Benki ya dunia


Kulingana na mchambizi wa masuala ya siasa kutoka Tanzania Deus Kibamba benki hiyo hutazama pato la taifa kwa mfano kupitia jumla ya utajiri wa raslimali na ule wa kifedha na kugawanya na idadi ya watu wa Tanzania.

Amesema kwamba mataifa yenye kipato cha kati ya dola 1,006 hadi dola 3,955 kwa mtu mmoja hutajwa kuwa mataifa yenye kipato cha kati, lakini yaliyo na uchumi mdogo huku yale yenye kipato cha kati ya dola 3,956 hadi dola 12,235 yakidaiwa kuwa mataifa yenye kipato cha kati yenye uchumi unaoimarika.

Lakini je hii ina maana gani kwa taifa la Tanzania?


Kulingana na mchambuzi wa Tanzania Deus Kibamba, ni kwamba taifa hilo linaelekea kuimarika kiuchumi.

Kibamba anasema ni ishara kwamba siasa za taifa hilo zinaenda sambamba na ukuaji wa chumi wa taifa hilo na kwamba sifa hiyo italisaidia taifa hilo kuvutia uwekezaji zaidi wa kigeni hatua ambayo italifanya kuimarika zaidi kiuchumi.

Hatahivyo amesema kwamba Watanzania hawapaswi kufikiria kwamba mifuko yao tayari itaanza kufaidika kutokana na hilo, na badala yake akasema wanahitajika kufanya bidii zaidi ili kuboresha uchumi.
Sababu kuu zilizoifanya Tanzania kufikia uchumi wa kipato cha kati Sababu kuu zilizoifanya Tanzania kufikia uchumi wa kipato cha kati Reviewed by Zero Degree on 7/03/2020 12:27:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.