Loading...

Mambo yanayochangia kumiminika kwa watalii katika Hifadhi ya Ruaha



MAAJABU manne katika Hifadhi ya Taifa Ruaha yamechangia kwa kiasi kikubwa kuvutia watalii kutembelea na kujifunza aina mbalimbali za vivutio vilivyobarikiwa katika eneo hilo.

Maajabu hayo ambayo ndio upekee wa hifadhi hiyo unaifanya Hifadhi ya Ruaha kuendelea kupokea watalii kila wakati ambao wanashawishiwa kushuhudia uzuri huo.

Kwa mujibu wa Ofisa Uhifadhi Utalii Hifadhi ya Ruaha, Amina Salum miongoni mwa vivutio vya kipekee katika eneo hilo ni uwezekano wa kuwaona kwa wakati mmoja wanyama lesser na greater kudu kwa sababu ni eneo la mtawanyiko kwa wanyama hao.

Ameongeza kuwa uwezekano wa kuwaona swala aina ya palahala, korongo, tohe, nyumbu, Mbwa mwitu, simba, duma, nyati, tembo pundamilia na twiga.

Amesema hifadhi hiyo imejaaliwa kuwa na zaidi ya aina 574 za ndege wanaofanya makazi yao kwenye hifadhi hiyo na kuwa kivutio kikubwa kwa wageni kwa sababu utofauti wa uoto wa asili na mwinuko ndio visababishi vikuu kwa kuwepo kwa wingi wa aina tofauti za ndege hao.

“Kuwepo kwa utofauti mkubwa wa mwinuko kutoka mita 750 hadi 1868 huku kukiwa na mto Ruaha mkuu, mabonde na ardhi oevu za Usangu, tambarare za juu na milima kama Isunkaviola na kingo za mgawanyiko ni sifa nyingine ya hifadhi yetu ya Ruaha,” amesema Salum.

Ameeleza kuwa hifadhi ya Ruaha inapatikana kwenye makutano ya mimea na wanyama kutoka upande wa kaskazini na kusini mwa Afrika hivyo kuifanya kuwa na aina nyingi za wanyama na mimea.

Amesema Uoto wa asili hutofautiana kutoka tambarare za mto ruaha ambapo ni nyika za wazi huku zikibadilika kuwa misitu ya miombo na kufikia kwenye kingo za tambarare zinazopatikana juu ya milima zikiwa na uoto tofauti kabisa huku bonde uevu la Usangu linatoa uoto wa kipekee hivyo kuwavutia wageni.

Amesema licha ya uwepo wa ugonjwa wa Uviko 19 wageni ndani ya nchi wamekuwa na muitikio mkubwa kutembelea vivutio katika Hifadhi ya Ruaha kwa kutumia mbinu mbalimbali za kuhamasisha utalii kupitia vyombo vya habari na vipeperushi mbalimbali.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Halima Kiwango alisema Uhifadhi wa eneo hilo ulianza tangu mwaka 1910 wakati huo ikijulikana kama Pori la Akiba la saba.

Amesema mwaka 1946 Waingereza waliongeza eneo na kubadili jina kuita Pori la Akiba la Rungwe na baadae mwaka 1974 likatangazwa kama Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Ameongeza kuwa Hifadhi ya Ruaha inafikika kwa njia ya barabara kilomita 108 kutoka Mji wa Iringa ambayo inapitika mwaka mzima lakini pia kilomita 625 kutoka jijini Dar es Saalam na kilomita 480 kutoka jijini Mbeya.

Chanzo: Nipashe
Mambo yanayochangia kumiminika kwa watalii katika Hifadhi ya Ruaha Mambo yanayochangia kumiminika kwa watalii katika Hifadhi ya Ruaha Reviewed by Zero Degree on 11/03/2021 01:30:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.