Loading...

Bado hatujafika tunapotaka - Kocha Azam


Kocha wa Azam FC, amewaahidi mashabiki wa Azam soka la kuvutia kutoka nchini Morocco ambako amekuta timu nyingi zinapenda kuuchezea mpira.

Akizungumza kutoka nchini humo ambako kikosi cha timu hiyo kimepiga kambi kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa mashindano, Bruno Ferry, amesema ameona aina fulani ya soka nchini humo ambalo ni la kuvutia na ameanza kuliingiza kwenye kikosi chake kwani kina baadhi ya wachezaji ambao ni mafundi wa mpira miguuni.

"Nimeona soka la Morocco ni la kiufundi sana, wanapenda kuchezea mpira, nasi hatuna tatizo na hilo, tunao wachezaji ambao wanaweza kulicheza, kuna vitu ambavyo tunawaongezea wachezaji wetu ili waweze kucheza aina hiyo ya soka la kuburudisha na kuvutia machoni, huku wakisaka ushindi," alisema kocha huyo.

Jumamosi iliyopita, Azam FC, ilicheza mchezo wa kwanza wa kujipima nguvu dhidi ya US Yacoub Al Mansour inayoshiriki Ligi Daraja la Tatu nchini humo na kushinda mabao 3-0.

Akizungumzia maandalizi kwa ujumla, alisema bado wachezaji wake hawajafika anapopataka, lakini kazi inaendelea kuwafua ili wawe vizuri.

"Bado hatujafika tunapotaka, ila ni hali ya kawaida katika kipindi hiki cha maandalizi, kwa sasa ni muhimu kuendelea na mazoezi ya utimamu wa mwili, ni wakati wa kujiandaa na michezo mbalimbali na kuhakikisha wachezaji wapya wanaingia kwenye mfumo.

"Katika soka kuna hasi na chanya, tunajua kila kitu hakiwezi kuwa sawa na vile unavyotaka, vinahitaji muda, nadhani mashindano yatakapoanza tutakuwa tayari," alisema.

Mbali na Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam inajiandaa pia na Ligi ya Mabingwa Afrika, ilipangwa kucheza dhidi ya APR ya Rwanda kuanzia Agosti 16 na 18, mwaka huu kabla ya hapo inatakiwa kuikabili Coastal Union, Agosti 8 katika mechi ya Ngao ya Jamii, Uwanja wa New Amaan Complex, mjini Zanzibar.


Chanzo: Nipashe
Bado hatujafika tunapotaka - Kocha Azam Bado hatujafika tunapotaka - Kocha Azam Reviewed by Zero Degree on 7/23/2024 12:59:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.