Kibu Denis kukatwa nusu ya mshahara wake
Kuna jambo linaendelea juu ya sakata la mshambuliaji wa Simba, Kibu Denis kutokana na kuchelewa kujiunga na kambi ya kujiandaa na msimu wa 2024-2025 iliyopo Ismaili, Misri.
Simba ambayo ipo nchini humo tangu Julai 8, mwaka huu, ikijifua imekwenda na wachezaji wote itakaowatumia msimu ujao kasoro Kibu na Aishi Manula ambaye amekuwa majeruhi wa muda mrefu, lakini ni kama uongozi umemuweka kando kwanza licha ya kupona.
Kibu ambaye hivi karibuni aliongeza mkataba wa kuendelea kuichezea Simba kitendo cha kutojiunga na timu hadi sasa kimeibua mjadala na mwenyewe akionekana akila bata Marekani.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimeliambia Mwanaspoti kuwa, staa huyo ambaye msimu uliopita alifunga bao moja katika ligi dhidi ya Yanga uwezekano wa kwenda Misri kuungana na wenzake i mdogo, hivyo ana asilimia kubwa ya kuisubiri timu irudi Dar.
Kutokana na ishu hiyo, inaelezwa kuwa uongozi wa Simba unadaiwa kufikia uamuzi wa kumkata nusu mshahara kutokana na kushindwa kufika kambini kama ilivyotakiwa kwa nyota wote.
“Kibu kachelewa kujiunga na kambi na hakutoa taarifa mapema kuhusiana na shida aliyonayo. Kwa mujibu wa mkataba ni wazi kuwa mchezaji akichelewa kufanya hivyo anakatwa nusu ya mshahara wake,” kilisema chanzo hicho kutoka Simba na kuongeza:
“Kibu analipwa Sh10 milioni hivyo ni wazi atakatwa Sh5 milioni shahara wake wa mwezi wa kwanza wa mkataba mpya aliosaini na Simba.”
Mbali na kukatwa mshahara, chanzo kimedai kuwa sio rahisi kwa Kibu kwenda Misri kipindi hiki na zaidi ataungana na Simba jijini Dar es Salaam itakaporudi.
Kibu ambaye alikuwa mapumziko Miami Beach katika Jiji la Florida nchini Marekani, inaelezwa tayari amerejea Tanzania na yupo Dar es Salaam.
Juhudi za kumpata Kibu jana hazikuzaa matunda.
SIKU 16 HAYUPO KAMBINI
Mpaka leo Kibu amekosekana katika kambi ya Simba kwa siku 16. Ikumbukwe kwamba Simba ilifika Misri Julai 8 na inatarajiwa kurejea Dar mwishoni mwa mwezi huu kabla ya Agosti 3 kuwa na yamasha la Simba Day ambalo huambatana na utambulisho wa wachezaji watakaoitumikia msimu ujao.
Kuchelewa kwa mchezaji huyo kuingia kambini kunamfanya Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids kuendelea kuwanoa wengine wanaocheza eneo la ushambuliaji ambalo pia Kibu anacheza.
Chanzo: Mwanaspoti
Washambuliaji wa Simba kuelekea msimu ujao ni Jean Ahoua, Steve Mukwala, Valentine Mashaka, Freddy Michael na Kibu ambaye atakuwa na kazi ya ziada ya kufanya ili kuhakikisha anapenya kikosi cha kwanza baada ya kutokuwa kambini huku wenzake wakiendelea kujinoa.
Kibu Denis kukatwa nusu ya mshahara wake
Reviewed by Zero Degree
on
7/22/2024 06:24:00 PM
Rating: