Loading...

Rais William Ruto avunja baraza la mawaziri Kenya

Rais wa Kenya, William Ruto avunja baraza la mawaziri Kenya

Rais William Ruto amelivunja baraza lake la mawaziri na kuziacha nafasi mbili pekee-ya Kiongozi wa mawaziri na Waziri wa Masuala ya Kigeni Musalia Mudavadi na afisi ya naibu wa rais Rigathi Gachagua.

Amesema atachukua muda kufanya majadiliano ya kuunda baraza jipya la mawaziri litakalohusika na uendeshaji wa serikali.

'Mara moja nitashiriki katika mashauriano ya kina katika sekta mbalimbali na miundo ya kisiasa, kwa lengo la kuunda serikali pana ambayo itanisaidia katika kuongeza kasi na kuharakisha yanayohitajika, ya haraka pamoja na utekelezaji wa mipango mikali ya kukabiliana na mzigo wa madeni, kuongeza rasilimali za ndani, kupanua nafasi za kazi, kuondoa uharibifu wa fedha na marudio yasiyo ya lazima ya msururu wa vyombo vya serikali na kuua joka la ufisadi hivyo kuifanya serikali kuwa isiyo na gharama kubwa , na yenye ufanisi' ,rais amesema katika hotuba yake kwa taifa.

Rais Ruto amesema wakati akiendelea na mchakato wa kuliteua baraza jipya la mawaziri ,shughuli za serikali zitaendelea bila kuvurugwa chini ya uongozi wa Makatibu kudumu na maafisa wengine husika.

Mawaziri watatu kati ya waliofutwa kazi walikuwa wabunge kabla ya kuacha majukumu yao na kujiunga na baraza la mawaziri miaka miwili iliyopita.

Mmoja wao ni Aden Duale, ambaye katika chapisho la haraka kwenye X (zamani Twitter) alimshukuru rais na kusema "atakuwa na deni kwake na watu wa Kenya milele kwa fursa hii ya kuhudumu" kama waziri wa ulinzi wa Kenya.

Alhamisi iliyopita, Rais Ruto aliongoza kikao cha baraza la mawaziri ambacho gazeti moja la humu nchini lilieleza kuwa ni “Chajio cha mwisho” kwa mawaziri hao.

Baadhi ya mawaziri hao walihusishwa na kashfa za ufisadi zilizosababisha kusimamishwa kazi kwa maafisa wakuu wa serikali ndani ya wizara kadhaa. Lakini Bw Ruto alikuwa amewatetea akisema kuwa hakuna ushahidi wa kuwatimua.

Oktoba iliyopita, Bw Ruto alitangaza mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri yaliyoathiri takriban mawaziri wanane.

Mara ya mwisho kwa baraza zima la mawaziri kuvunjwa ilikuwa mwaka wa 2005 wakati Rais Mwai Kibaki alipofanya hivyo muda mfupi baada ya kushindwa katika kura ya maoni kuhusu katiba mpya.

Bw Ruto amekuwa chini ya shinikizo kutoka kwa Wakenya ambao wameendelea kufanya maandamano dhidi ya serikali na kutaka serikali iwajibike zaidi, ingawa alikubali kuondoa Mswada wa fedha uliozua utata.

Baadhi ya waandamanaji wamekuwa wakimtaka rais aondoke.

Wiki jana, Bw Ruto alitangaza hatua kadhaa za kubana matumizi katika mashirika mbalimbali ya serikali.

Pia aliamuru kusitishwa kwa mapendekezo ya nyongeza ya mishahara kwa baraza lake la mawaziri na bunge kufuatia malalamiko hayo.

Ruto amesema uamuzi huu ulichukuliwa baada ya matukio ya hivi majuzi nchini Kenya ambayo yalilazimu kuondolewa kwa Mswada wa Fedha wa 2024 na baada ya "kutafakari, kusikiliza Wakenya, na baada ya tathmini ya jumla ya baraza langu la mawaziri".

Katika hotuba yake akiwa Ikulu ya Nairobi,Ruto alitangulia kwa kueleza baadhi ya mafanikio ya serikali yake kwa muda wa miaka miwili ikiwemo kupunguza mfumko wa bei za bidhaa,kuifanya thabiti shilingi ya Kenya dhidi ya dola ya Marekani,kuunda nafasi zaidi za ajira kupitia vituo vya kidijitali na mpango wa ujenzi wa nyumba na kupunguza bei ya mbolea kwa wakulima.

Hatua hiyo ya hivi punde ya Ruto imejiri baada ya wiki kadhaa za msururu wa matukio nchini Kenya ambayo yametikisa nchi hiyo ya afrika mashariki.

Maandamano ya vijana wa kizazi cha Gen Z kuishinikiza serikali kuwajibika zaidi kupitia utawala bora na matumizi mazuri ya fedha za umma kando na kuukataa mswada wa fedha ,yamechangia mwelekeo mpya wa serikali ya rais ruto.

Kando na kufaulu kuishinikiza serikali kuufuta mswada wa fedha wa 2024 ,maandamano hayo ya vijana pia yamemfanya Ruto kutangaza hatua mbalimbali za kupunguza matumizi ya serikali ikiwemo kuondoa bajeti kwa afisi za mke wa rais na mke wa naibu wa rais kando na kubana matumizi ya fedha za ofisi yake na nyingine za umma.

Maafisa wa serikali pia wamepigwa marufuku dhidi ya kushiriki katika hafla za kuchangisha fedha ,harambee ili kuzuia ufujaji wa fedha za umma.

Mtihani mkubwa kwa Rais Ruto sasa utasalia kuwaridhisha Wakenya wengi ba baraza jipya atakaloliteua. Kuwarejesha mawaziri waliotenguliwa kutoka wizara moja hadi nyingine huenda ni hatua ambayo itazua lalama zaidi kulingana na wadadisi.

Pia wengi wanasubiri kuona iwapo idadi ya mawaziri itapunguzwa ili kubana matumizi ya fedha za umma kama alivyohidi katika siku za hivi karibuni alipokariri umuhimu wa kuwa na serikali isiyokuwa ya kuharibu raslimali za umma kupitia nyadhifa nyingi za ngazi ya juu.
Rais William Ruto avunja baraza la mawaziri Kenya Rais William Ruto avunja baraza la mawaziri Kenya Reviewed by Zero Degree on 7/12/2024 06:30:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.