Loading...

Serikali yatangaza ajira 11,015 za walimu


Serikali imetangaza nafasi za ajira 11,015 za sekta ya elimu, ikiwa ni baada ya kuwapo kwa ahadi kadhaa za kuajiri walimu 12,000 katika mwaka wa fedha 2024/25.

Ahadi hizo zilitolewa kwa nyakati tofauti na baadhi ziliahidiwa bungeni, jijini Dodoma.

Baadhi ya ajira zilizotangazwa zimeelekezwa kwa masomo ya kemia, fizikia na biolojia katika ngazi ya ualimu daraja la IIIB na IIIC, huku wale wa hisabati wakiwa zaidi ya 1,325.

Ajira hizo zimetangazwa wakati takwimu zinaonyesha madarasa ya awali na msingi pekee yanahitaji walimu zaidi ya 116,885 ili kuweka uwiano sawa wa walimu kwa wanafunzi.

Kwa mujibu wa kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa 2023 kilichotolewa na Wizara ya Fedha, kwa udahili uliofanyika mwaka jana, madarasa ya awali yalihitaji walimu 52,884 na shule za msingi zilihitaji walimu 64,001 ili kuwa na uwiano uliopangwa na Serikali pindi walimu hao watakapojumuishwa na waliopo shuleni.

Hiyo ikiwa na maana kuwa walimu 11,015 waliopangwa kuajiriwa ikiwa wote wangeelekezwa katika shule za awali na msingi pekee, ingekuwa ni sawa na kupunguza uhaba kwa asilimia 9.42.

“Ni hatua inayopaswa kupongezwa, lakini jitihada zaidi zinatakiwa kufanyika kuziba pengo lililopo, kwani walioajiriwa ni wachache na wanaohitajika ni wengi,” amesema Muhanyi Nkoronko, mtafiti wa elimu.

Muhanyi amesema ajira zilizotolewa zitasaidia kupunguza pengo linalosababishwa na upungufu wa walimu hasa baada ya kuwapo ongezeko la wanafunzi lililosababishwa na elimu bure.

“Kwa kiasi itapunguza changamoto katika ufundishaji na kuwapo kwa mabadiliko kidogo, walau wanafunzi wanaweza kupata maarifa stahiki, mwalimu anaweza kuongezewa uwezo wa kumfikia mwanafunzi mmoja mmoja, jambo litakaloongeza ubora kwenye ufundishaji,” amesema.

Ajira hizo pia zitasaidia kupunguza mzigo kwa walimu kupitia idadi ya wanafunzi anaowafundisha, wataweza kujiandaa vyema, kuandaa maandalio yao kabla ya kufundisha.

(Kuomba ajira bofya hapa)


Dirisha la maombi ya ualimu limefunguliwa baada ya kufungwa la sekta ya afya ambalo lililenga kutafuta watumishi 9,483. Lilifunguliwa Julai 7, 2024 na kufungwa Julai 20, 2024.

Ajira za walimu zimegusa masomo yote yakiwamo kemia, biolojia na fizikia ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakilalamikiwa kutokana na kuwa na walimu pungufu. Mbali ya hao, zimewagusa mafundi sanifu kwa ajili ya maabara nchini.

Pia kuna ajira za walimu wa masomo ya biashara, elimu maalumu, jiografia, Kiingereza, fasihi ya Kiingereza, Kiswahili, historia, uraia, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), kilimo, Kifaransa, lishe, ushonaji na uchumi.

Mdau wa elimu, Alistidia Kamugisha amesema hiyo ni hatua nzuri inayopaswa kupongezwa, kwani ni ngumu kuhesabu 10 bila kuanza na moja.

“Serikali ni baba wa watoto wengi, ajira zikiendelea kutolewa polepole tutamaliza uhaba,” amesema Kamugisha.

Hata hivyo, ametaka kipaumbele kitolewe kwa walimu waliojitolea, kwani baadhi wamefanya kazi zaidi ya miaka minne katika shule mbalimbali na kuwa sehemu ya mafanikio.

Mhadhiri wa elimu kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Luka Mkonongwa amesema kitendo cha kutangaza ajira hizo hata kwa uchache ni ishara kuwa Serikali imekubali kuwapo uhaba wa walimu.

“Pia imetambua wapo watu waliomaliza shule, waliwekeza kwenye elimu lakini elimu yao haijawalipa, ni hatua nzuri,” amesema.

Ametaka kuendelea kusimamiwa viwango vya ubora wa elimu kwa kujenga kesho iliyo bora.
Amesema hilo lifanyike kwa kutoa ajira kwa walimu wenye sifa na uwezo wa kufundisha ngazi mbalimbali kulingana na dunia ya sasa ilivyo.

Mei 9, 2024 akiwa bungeni jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Zainab Katimba alisema mwaka wa fedha 2024/25 walimu 12,000 wataajiriwa na watapangiwa vituo vya kazi katika maeneo yenye upungufu.

Ajira hizo ni mwendelezo wa kinachofanyika katika kupunguza uhaba wa walimu uliopo, akifafanua kati ya mwaka 2020/21 hadi 2022/23 Serikali iliajiri walimu 29,879 wakiwemo 16,598 wa shule za msingi na 13,281 wa shule za sekondari.

Ajira zilizotolewa awali


Mwaka 2021 Serikali ilianza kutoa ajira kwa walimu ikiwa ni baada ya kusitishwa kwa miaka kadhaa.

Katika kupunguza pengo la walimu lililokuwapo, Juni 2021 walimu 6,949 waliajiriwa kati yao 3,949 walikuwa wa shule za msingi na 3,000 wa sekondari.

Baadaye Juni, 2022 walimu 9,800 waliajiriwa kati yao 5,000 walikuwa wa shule za msingi na 4,800 wa sekondari.

Mwaka jana, walimu 13,130 wa shule za msingi na sekondari waliajiriwa.

Serikali yatangaza ajira 11,015 za walimu Serikali yatangaza ajira 11,015 za walimu Reviewed by Zero Degree on 7/23/2024 11:22:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.