Loading...

Tuna kila sababu ya kuyashukuru makanisa kwa kuunga mkono juhudi za Serikali - Wziri Mkuu

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amezitaka taasisi za dini nchini kuendelea kushirikiana na serikali

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amezitaka taasisi za dini nchini kuendelea kushirikiana na serikali kutoa mchango kwenye maendeleo ya taifa.

Amesema kuwa taasisi za dini zina uwezo mkubwa wa kutoa huduma imara za kiroho na kugusa maisha ya watu katika jamii na kuwaletea maendeleo ya kiuchumi na kisiasa.

Majaliwa alitoa wito huo jana kwenye Kilele cha Mkutano wa Baraza la Maaskofu wa Makanisa ya Pentekoste Tanzania (CPCT), uliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Biblia Miyuji, jijini Dodoma.

“Tuna kila sababu ya kuyashukuru makanisa kwa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuleta maendeleo ya wananchi kwa ujumla, yamekuwa sehemu ya suluhisho katika changamoto za kijamii kama vile umaskini, elimu duni, na matatizo ya kiafya.

“Nitumie fursa hii kusisitiza taasisi za dini kuendelea kuimarisha ushirikiano na serikali na kuendelea kuiishi kwa vitendo kaulimbiu yenu ya Palipo na Umoja, Bwana Huamuru Baraka! Bwana Huamuru Baraka Palipo na Umoja,” alisema.

Katika hatua nyingine, Majaliwa alisema serikali inathamini mchango wa taasisi za dini katika kuhubiri amani na utulivu nchini.

“Siri ni ya haya yote ni sababu ya uwapo wa dini katika kuhubiri maadili, mshikamano, upendo uvumilivu na kuwa wamoja, serikali pekee tusingeweza,” alisema.

Mwenyekiti wa CPCT, Askofu Dk. Barnabas Mtokambali, alisema baraza hilo kupitia madhehebu wanachama wake, litaendelea kushirikiana na serikali katika kuendeleza sekta za elimu, na afya nchini kwa kujenga na kuendesha hospitali, vituo vya afya, shule na vyuo vya aina mbalimbali.

“Hili si tu kwamba linapunguza mzigo mkubwa wa serikali katika kuihudumia jamii kubwa ya Watanzania katika mahitaji husika, bali pia linasaidia kupunguza tatizo kubwa la ukosefu wa ajira kwa vijana,” alisema.

Aliongeza kuwa CPCT itaendelea kushirikiana na serikali katika kuhimiza maadili mema kwa mafundisho ili kupinga wimbi la mmomonyoko wa maadili linaloukumba ulimwengu mzima.

“Baraza limekuwa mstari wa mbele kupinga vitendo kama ndoa za jinsia moja, ushoga, kutokuwajibika kwa wazazi kutunza familia kunakosababisha kuongezeka kwa watoto wa mitaani, mila potofu za ukeketaji wanawake, imani za kishirikina zinazopelekea watu wenye ulemavu wa ualbino kuuawa kwa dhana,” alisisitiza.
Tuna kila sababu ya kuyashukuru makanisa kwa kuunga mkono juhudi za Serikali - Wziri Mkuu Tuna kila sababu ya kuyashukuru makanisa kwa kuunga mkono juhudi za Serikali - Wziri Mkuu Reviewed by Zero Degree on 7/20/2024 07:14:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.