Tunao umeme wa kutosha - Rais Samia
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa kwa sasa nchi inao umeme wa kutosha |
📌Asema Rukwa kuungwa kwenye Gridi sambamba na Katavi na Kigoma mwezi Oktoba
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema kuwa kwa sasa nchi inao umeme wa kutosha kufuatia miradi mbalimbali ambayo Serikali imetekeleza ukiwemo ule wa JNHPP kwa kuwashwa mashine mbili ambazo zinaendekea kufanya kazi.
Mhe. Dkt. Samia ameyasema hayo wakati alipokutana na wazee wa mkoa wa Rukwa ikulu ndogo mjini Sumbawanga, wakati wa ziara yake mkoani Rukwa kukagua maendeleo ya utekelezaji miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali ikiwa ni mwanzo wa ziara yake ya siku tatu mkoani humo.
‘’Nipende kuwahakikishia watanzania kuwa kwa sasa tunao umeme wa kutosha na tunakwenda kuufungua mkoa wa Rukwa kiuchumi kwa kuhakikisha unaungwa kwenye Gridi ya Taifa sambamba na Kigoma na Katavi’’ Alisema Mhe.Dkt. Samia.
Amesema uwepo wa umeme wa kutosha na uhakika utasaidia kufungua fursa za uwekezaji na kuishukuru Wizara ya Nishati kwa kazi kubwa inayofanywa kupitia TANESCO kwenye utekelezaji wa miradi hiyo.
Akiwasilisha risala ya wazee wa mkoa wa Rukwa kwa niaba yao, mwenyekiti wa wazee hao mzee Timoth Makaza, amemuomba Mhe. Dkt. Rais Samia kuondoa tozo kwenye vifaa, Teknolojia na mitungi ili kuwawezesha wazee kuunga mkono jitihada za Serikali kutumia Nishati safi ya kupikia na kuomba kushusha bei ya Nishati hususani kwa wananchi wanaoishi vijijini.
Akijibu hoja mbalimbali za wazee hao, Mhe. Dkt. Samia amesema Nishati safi ya kupikia ni muhimu kwa wananchi wote ili kutunza mazingira pamoja na misitu.
Hivi karibuni Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na taasisi za Serikali imeunda timu inayoendelea kufanya mapitio ya Sheria, Sera na Kanuni zinazohusu masuala ya nishati safi ya kupikia ikiwa ni pamoja na tozo na kodi, ili Kuleta unafuu kwenye nishati safi ya kupikia kwa watumiaji.
Tunao umeme wa kutosha - Rais Samia
Reviewed by Zero Degree
on
7/16/2024 10:01:00 AM
Rating: