Loading...

Wamisri waitega Simba.

Mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajibu.
BIASHARA ya mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajibu kwenda Haras El Hodoud ya Misri inaelekea kutokamilika kwa sasa.

Dirisha la usajili la Misri lilifungwa jana na Haras El Hodoud hawakuwa wamefanya mawasiliano yoyote na Simba hadi jana jioni na haifahamiki endapo jina la Ajibu lipo katika orodha ya wachezaji waliosajiliwa na klabu hiyo ikisubiri kumalizana na Simba na kupata Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) au la.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba, Hajji Manara alisema jana katika mazungumzo na Nipashe kuwa klabu yake haijapokea ofa yoyote kutoka kwa Haras El Hodoud.

“Sijui wanategemea nini, maana dirisha la usajili la kwao linafungwa leo (jana). Sasa sijui wana mpango gani,”alisema Manara.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Ajibu ambaye mkataba wake na Simba unamalizika mwishoni mwa msimu, alisema amefanya mazungumzo ya awali na Haras El Hodoud na kufikia makubaliano, lakini kwanza wanatakiwa kumalizana na klabu yake.

“Ninamshukuru Mungu nimefurahia siku zangu chache za kuwa Alexandria, nilikuwa katika klabu nzuri, mazingira mazuri na wachezaji wenzangu kule wamenikubali mapema sana. Sasa baada ya yote, ninawasikilizia wao tu ni jinsi gani watalimalizia hili suala,”alisema.

Ajibu alirejea nchini juzi na kusema kwamba atajiunga na timu itakayompa ofa nzuri kati ya Haras El Hodoud ya Misri na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini inayomtaka pia.

Pamoja na kufuzu majaribio na vipimo vya afya Haras El Hodoud, lakini imeripotiwa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini pia inamtaka mchezaji huyo wa Simba kwa kusaini naye mkataba moja kwa moja bila majaribio.

“Ni kweli nimesikia hizo habari, na si Kaizer tu, timu nyingine kama mbili za Afrika Kusini nazo zimetangaza ofa. Kwanza ninamshukuru Mungu. Mungu ni mkubwa, sasa tusubiri haya maneno yawe vitendo ndiyo tufanye maamuzi,” alisema.

Wakala anayeshughulikia mipango ya Ajibu nchini Afrika Kusini, Rodgers Mathaba kwa upande wake alikiri juu ya mchezaji huyo kutakiwa na Kaizer Chiefs.

“Ni kweli, Kaizer wanamtaka Ajibu. Najua alikuwa Misri, nasubiri arejee Dar es Salaam nimpigie simu nizungumze naye. Tayari nimekwishazungumza na kocha Steve Khompela wa Kaizer,”alisema.

Ajibu alikuwa na wiki nzuri ya majaribio Haras El Hodoud ikiwamo kufunga bao moja katika ushindi wa 4-0 kwenye mchezo wa kirafiki Ijumaa. 

Mathaba ndiye aliyempeleka Ajibu Afrika Kusini kwa majaribio pia, katika klabu ya Lamontville Golden Arrows FC ya Ligi Kuu ya ABSA, kwani pamoja na kufuzu, walimtaka arejee Simba kumalizia mkataba ili baadaye wamsajili kama mchezaji huru.

Source: Nipashe
ZeroDegree.
Wamisri waitega Simba. Wamisri waitega Simba. Reviewed by Zero Degree on 1/03/2017 06:38:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.