Loading...

Bajeti yapita kwa asilimia 73


BAJETI ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/18 ya Sh trilioni 31.7, imepitishwa kwa asilimia 73 ya kura zilizopigwa na wabunge jana baada ya majadiliano ya siku saba.

Katika upigaji kura, kura za Ndiyo zilikuwa ni kura 260 kati ya 355 zilizopigwa huku kura za Hapana zikiwa 95. Hakukuwa na kura iliyoharibika. Katika kura ambazo zimepigwa jana bila kura ya uamuzi ya Spika, kura 258 ni za wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) huku kura mbili zikitoka kwa wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF), za Jimbo la Mtwara Mjini, Maftah Nachuma na Magdalena Sakaya wa Kaliua.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge wa CCM waliomba Mwongozo wa Spika wakitaka fedha za maendeleo zilizopitishwa katika Bunge hilo zisipelekwe kwa wabunge ambao wamepiga kura ya hapana. “Kama wamekataa bajeti, inamaanisha watu wenu hawana matatizo na hivyo hamuhitaji fedha hizo,” alisema Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku Msukuma (CCM), huku Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu, Jenista Mhagama aliomba mwongozo kama kuna sababu ya mbunge aliyepiga kura ya kukataa bajeti, kuhoji serikali kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Hata hivyo, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema) alipinga hoja za wabunge waliopiga kura za hapana wasipewe fedha hizo kwa sababu fedha za maendeleo sio hisani, bali ni kodi ya wananchi. Aidha, Bunge limepitisha Sheria ya Matumizi ya Fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwa Mwaka wa Fedha 2017/18. Akihitimisha mjadala wa Taarifa ya Hali ya Uchumi 2016 na Bajeti ya Serikali 2017/18 aliyoiwasilisha Juni 8, mwaka huu, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alitangaza kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa magari ya kubeba wagonjwa, leseni na ada za uwindaji, lengo likiwa ni kukuza biashara katika sekta hiyo.

Pia Dk Mpango alitangaza kufuta VAT katika ada ya tathmini ya mazingira kwa wawekezaji wote wa viwanda na tozo na ada za zimamoto kwa shule binafsi, akiwa na matumaini wamiliki wa shule wataweka muundo wao wa ada ili kuwa watoto wa Tanzania wapate elimu kwa unafuu. Aidha, kuanzia Julai mosi, mwaka huu, mapato yote yatakayotokana na michezo ya kubahatisha yatakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Akifafanua kuhusu kodi ya majengo, Dk Mpango alisema nyumba zilizojengwa kwa udongo na zilizoko vijijini na huku nyumba zinazomilikiwa na wenye nyumba walizojenga na kuishi watu wenye umri wa miaka 60 kwa mjini na vijijini, hazitahusika katika kulipa kodi hiyo. “Kodi ya majengo itahusu nyumba zilizojengwa katika majiji, miji na miji midogo, nyumba zilizoko vijijini na zile za tope hazitalipiwa kodi na linakwenda sambamba na nyumba ambazo ni za kuishi watu wenye umri wa miaka 60 na kuendelea,” alifafanua Dk Mpango.

Akifafanua zaidi tozo ya Sh 10,000, kwa nyumba ambazo hazijathaminiwa hususani za vijijini, pamoja na tozo ya Sh 50,000 kwa ghorofa ambazo wanaishi wastaafu, Dk Mpango alisema kodi ya majengo hutozwa kwa mujibu wa Sheria za Mamlaka za Miji Sura ya 289 Bajeti yapita kwa asilimia 73 Kifungu cha Pili cha Sheria za Mamlaka za Miji, inabainisha kuwa kodi ya majengo inatozwa kwenye majengo yaliyojengwa kwenye mamlaka za mijiji, miji na mamlaka za miji midogo.

Wakati wa mjadala, wabunge walibainisha kuwa kutoza Sh 10,000 na Sh 50,000 kwa nyumba za vijijini na tembe ni kutowatendea haki watu hao. Hata hivyo, Dk Mpango alisisitiza kuwa kodi ya majengo itakusanywa na TRA, ikiwa ni tofauti na hoja za baadhi ya wabunge kwa kutaka kodi hiyo kukusanywa na halmashauri kwani ni kuzinyang’anya halmashauri hizo vyanzo vya mapato.

Alisema ili kuwahamasisha wafanyabiashara wadogo kurasimisha shughuli zao na serikali ikusanye kodi, utaratibu alioutangaza kuhusu kuwatambua wafanyabiashara wa aina hiyo na kuwapa vitambulisho, utahusisha pia washereheshaji (MC), watoa huduma za chakula, na wafanyabiashara wadogo wasio rasmi wanaofanya biashara katika maeneo rasmi. Alisema wabunge 193 walichangia mjadala wa bajeti na kwamba serikali imepokea michango mingi na ushauri kwa maendeleo ya taifa, ambapo baadhi wanaifanyia kazi kwenye bajeti hii na mingine katika bajeti ijayo.

“Naungana na wabunge wote waliompongeza Rais John Magufuli kwa kulinda rasilimali za taifa na kuhakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali zao,” alisema Dk Mpango na kutangaza kuwa serikali imefanya marekebisho katika Sheria ya VAT ili kusamehe kodi hiyo kwenye magari ya kubeba wagonjwa (ambulance). “Hatua hiyo itahusisha magari yanayoingizwa nchini yakiwa yametengenezwa mahususi kwa ajili ya kubeba wagonjwa na kwamba yanaingizwa nchini kwa matumizi ya hospitali au vituo vya afya vilivyosajiliwa kisheria.”

Aliongeza: “Serikali itatumia utaratibu wa hati za malipo ya hazina katika kusimamia misamaha hii ambapo kodi inayosamehewa italipiwa na serikali kupitia Hazina kama inavyofanyika katika taasisi za dini ili kudhibiti matumizi mabaya ya misamaha hiyo.” Kuhusu kuondoa VAT kwenye ada ya vibali vya uwindaji vitolewavyo na serikali, alisema hatua hiyo inalenga kuhamasisha ukuaji wa shughuli za uwindaji na sekta ya utalii kwa ujumla.

Kuhusu marekebisho ya EPOCA, Dk Mpango alisema amependekeza kufanya marekebisho kwenye sheria hiyo ili hisa za asilimia 25, zitakazouzwa na kampuni ya mawasiliano kwenye soko za hisa ziuzwe kwa umma ili kuwezesha watanzania, kampuni za kitanzania wananufaika na hali hiyo. Akizungumzia utozaji tozo kwenye vyombo vya uvuvi kwa kutumia fedha za kigeni kwa vyombo vilivyosajiliwa nchini, Dk Mpango alisema kuanzia sasa serikali inaagiza taasisi zote zinahusika na tozo hizo ziache utaratibu huo mara moja na zianze kutoza tozo kwa shilingi ya Tanzania.

“Serikali imeona kuna uwezekano wa kuweza kupata mapato kwenye michezo ya kubahatisha, hivyo kuanzia Julai mosi, mwaka huu, mapato yote yatakayotokana na michezo ya kubahatisha yatakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),” alieleza na kuongeza kuwa ushauri uliotolewa na wabunge wengi katika maeneo mbalimbali, serikali inaangalia jinsi ya kuyazingatia mawazo hayo.

Aidha, alisema serikali itaendelea na kasi ya kutekeleza miradi ya maji mjini, kuboresha kodi ya majengo, kukamilisha utaratibu mzuri wa utoaji Sh milioni 50 kila kijiji, kulipa madeni ya wakandarasi na kudhibiti mfumko wa bei, pamoja na kudhibiti kuporomoka kwa shilingi. Alisema hoja kubwa iliyotawala mjadala wa bajeti mwaka huu, ni wabunge wengi walishauri kuongeza tozo ya Sh 50 kwa kila lita moja ya mafuta ili ikasaidie sekta ya maji hususan vijijini.

Mpango alisema katika mjadala, pia kulikuwa na hoja ya kodi na tozo nyingi zipatazo 16 zilizokuwa zikitozwa kwa shule binafsi, ambapo alibainisha kuwa serikali imesikia maoni na kuondoa baadhi ya tozo hizo. Naye Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji alilihakikishia Bunge kuwa serikali imejipanga kuhakikisha ahadi ya Rais Magufuli ya Sh milioni 50 inatekelezwa na kuwa wameshapanga Sh bilioni 120 kwa ajili ya kazi hiyo.

Pia Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe akichangia katika hitimisho hilo alisema wale wanaokosoa taarifa za kamati za kuchunguza makinikia, ni mamluki
Bajeti yapita kwa asilimia 73 Bajeti yapita kwa asilimia 73 Reviewed by Zero Degree on 6/21/2017 03:14:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.