Loading...

Ahadi ya Elimu bure haijaeleweka, soma hapa ufafanuzi kutoka kwa Naibu Waziri wa Elimu.


Naibu Waziri wa Elimu, Stella Manyanya.


Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Elimu, Stella Manyanya amesema, mpango wa Serikali wa kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi Kidato cha Nne hauwaondolei wazazi majukumu ya msingi kuhakikisha watoto wanapata elimu bora.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu, Manyanya (pichani) alisema sera ya elimu bure inalenga kuwapunguzia mzigo wazazi hasa wa gharama kama ada ambazo awali walikuwa wakilipa serikalini.

“Nadhani watu hawajaelewa. Zamani elimu ilikuwa ikitolewa kwa ubia kati ya Serikali na mzazi, kila upande una jukumu la kufanya kwa ajili ya elimu ya mtoto. Serikali ilikuwa inamlipa mwalimu na kukusanya Sh20,000 kwa wanafunzi wa kutwa na Sh70,000 kwa wanafunzi wa bweni,” alisema na kuongeza kuwa:

“Tuliposema elimu bure, maana yake sasa ile Sh 20,000 na Sh 70,000 zilizokuwa zinakusanywa na Serikali, tumesema sasa mzazi asitoe tena na hiyo imesaidia sana maeneo ya vijijini ambako wazazi walishindwa kulipa ada hiyo. Haikumaanisha kwamba sasa mzazi asiwe na jukumu kabisa katika elimu ya mtoto wake.”

Manyanya alisema itashangaza kama kuna wazazi ambao hawatawajibika kwa masuala ya msingi kabisa ya mtoto kupata elimu wakiitegemea Serikali kufanya kila kitu.

“Kama shule haina madawati, watoto wanakaa chini na wazazi wako tayari kuchangia, kwa nini wasichangie” alihoji Manyanya

Dhana ya elimu bure ambayo utekelezaji wake unasimamiwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, inazingatia uendeshaji wa shule bila ada wala michango ya aina yoyote ya lazima kutoka kwa wazazi ama walezi

Dhana hii ni utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015.

Elimu bora

Wakati dhana ya elimu bure ikiendana na ubora wa elimu hasa kukuza kiwango cha ufaulu, Manyanya alisema Serikali imeanza mchakato wa kuwakagua wakaguzi wa shule na kuwabana wasiotekeleza wajibu wao ipasavyo.

Pia aliwatangazia kiama baadhi ya walimu wanaozembea kufundisha kwa kisingizio cha kulipwa mishahara midogo, jambo linalochangia kushuka kwa kiwango cha elimu nchini.

Alisema Serikali haitawavumilia walimu na wakaguzi wa aina hiyo na kwamba wanaandaa mapendekezo ya kubadilisha baadhi ya sheria zinazoruhusu mlolongo mrefu wa namna ya kuwashughulikia kinidhamu watumishi.

“ Kama wakaguzi watafanya kazi kwa ufasaha, watagundua na kuvumbua yanayofanyika shuleni, kwa hakika kiwango cha elimu kitaongezeka. Idara hii ikiyumba, elimu nayo itayumba,” alisema.

Alisema kila mkaguzi atatakiwa kutoa taarifa ya ukaguzi wake na kufanyiwa kazi kwa kiwango cha juu ili kujiridhisha kama ina uhalisia na kama italeta mabadiliko.

Kuhusu walimu, Mhandisi Manyanya alisema wapo walimu wachache wazembe na wasiotekeleza wajibu wao kwa maksudi wakilalamikia kuwa mishahara ni midogo.

“Ni vibaya na hatari kupokea mshahara ambao unausema mdogo na kwa sababu hiyo hutaki kufundisha, kuna walimu wengi hawajaajiriwa na ikiwa unaona haukutoshi ni vizuri ukawapisha wenzako,” alisema na kuongeza;

“Hakuna kitu kibaya kama kudharau na kutoheshimu kazi yao eti kwa kuwa unalipwa kidogo; ukiona darasa unalofundisha wanafunzi hawakuelewi na mitihani yako wanafeli, jiulize mara mbili,”alisema.


ZeroDegree.
Ahadi ya Elimu bure haijaeleweka, soma hapa ufafanuzi kutoka kwa Naibu Waziri wa Elimu. Ahadi ya Elimu bure haijaeleweka, soma hapa ufafanuzi kutoka kwa Naibu Waziri wa Elimu. Reviewed by Zero Degree on 1/19/2016 08:02:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.