Loading...

Kifo cha Mtunzi wa Tamthiliya ya Ngoswe Penzi kitovu Cha Uzembe chatikisa sanaa.


Marehemu Edwin Semzaba, mtunzi wa kitabu cha Ngoswe.

Dar es Salaam. Kijana Ngoswe, ofisa muhesabu watu kutoka jijini Dar es Salaam, anafika kijijini akiwa amebeba mikoba miwili.



Mmoja una nguo zake na mwingine una vifaa vya kuhadidia watu. Amechoka baada ya mwendo mrefu. Anamuona mama mmoja akilima. Anasimama na kuweka chini mikoba yake. Anapangusa jasho na kuanza kujisemea mwenyewe.

Ngoswe: Kama mtu anasema shamba, basi shamba ndiyo hii. Loo! (akitazamatazama huko na huko). Vumbi jekundu kama ugoro wa subiani! Ama kweli nimefika. (Anainama na kuanza kuibenjua suruali yake ya aina ya “bell-batton”. Anaita): Mama!

Hivi ndivyo tamthiliya maarufu na ya kusisimua ya “Ngoswe: Penzi Kitovu cha Uzembe” inavyoanza.

Lakini sanaa ya uandishi huu, haitaonekana tena; Edwin Semzaba, mwandishi wa tamthiliya hiyo inayotumika kwenye somo la fasihi katika shule za sekondari, amefariki dunia.

Kitabu hicho, alichoandika akiwa mwanafunzi wa kidato cha pili Shule ya Sekondari ya Kigoma, kilimpa umaarufu kutokana na kuwa na staili yake, visa alivyoviweka ndani, maudhui yaliyoendana na enzi za mwanzoni mwa kujitawala na mchango wake kwenye fasihi.

Kabla ya kufariki, Semzaba alisema katika mahojiano na gazeti la The Citizen kuwa kitabu hicho kilimpa umaarufu kiasi cha kupona kuandikiwa faini ya Sh90,000 alipokamatwa na askari wa usalama barabarani baada ya mmoja wao kukumbuka jina lake kuwa ndiye mtunzi wa tamthiliya ya Ngoswe ambayo aliifanyia mtihani wa kidato cha nne na kufaulu.

Tamthiliya hiyo pia ilitengenezewa mchezo wa redio uliokizidishia umaarufu kitabu hicho, huku mtaani kukiwa na msemo wa “Mambo ya Ngoswe, muachie Ngoswe”.

Tamthiliya hiyo, ambayo aliiandika kutokana na uzoefu alioupata wakati aliposhiriki kazi ya kuhesabu watu mwaka 1967, inamuhusu kijana aliyeenda kijijini kufanya kazi ya sensa, lakini akatumbukia kwenye ulevi na mapenzi yaliyosababisha ashindwe kumalizia kazi baada ya kutaka kumtorosha binti aitwaye Mazoea, ambaye mzazi wake alibaini na akaamua kuchoma moto karatasi zote alizotumia.

Habari za kifo chake zilipokelewa kwa hisia tofauti na wadau wa sanaa, baadhi wakisema pengo lake halitazibika na wengine wakisema Semzaba amefariki, lakini kazi zake zitaendelea kuishi.

Dk Mona Mwakalinga, ambaye ni mkuu wa Idara ya Sanaa na Sanaa za Maonyesho ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anasema Semzaba, ambaye alikuwa mwalimu wa sanaa kwenye idara yake, ameacha pengo kubwa.

“Watu wanasema halizibiki, ni kweli na wala hatutataka lizibike kwa sababu hautampata Semzaba mwingine,” alisema Dk Mwakalinga.

“Semzaba alikuwa mmoja tu.”

Lakini akasema uongozi wa idara hiyo unashukuru kwa kupata nafasi ya kuwa naye chuoni hapo.

“Tumejifunza mengi sana kutoka kwake,” alisema Dk Mwakalinga ambaye aliwahi kuwa mwanafuzi wa Semzaba.

Alisema Semzaba alistaafu mwaka jana baada ya kufanya kazi chuoni hapo kwa zaidi ya miaka 10, waliandika barua ya kuomba aendelee kufanya nao kazi lakini kwa bahati mbaya wamempoteza kabla ya mchakato huo kukamilika.

Alisema Semzaba atakumbukwa siyo kwao tu bali hata kwenye shule za sekondari, vyuo vingine na hata nje ambako kazi zake zinatumiwa kwa shughuli za kitaaluma.

Dk Mwakalinga alizitaja baadhi ya kazi za marehemu kuwa ni mchezo wa kuigiza wa “Tende Hogo”, “Kinyamkera” na riwaya “Joseph na Josephine”.

“Tutazidi kuwa naye kwa hizo kazi zake. Pia tutazidi kukumbuka ucheshi wake na urafiki ambao alikuwa nao kwa kila mtu. Mtu ambaye huwa na furaha kila wakati, wala huwezi kumwona amekasirika.”

Kwa upande wake, mkufunzi wa idara hiyo, Richard Ndunguru alisema kifo cha Semzaba ni pigo kwani alikuwa na kipaji cha pekee katika kufundisha uandishi wenye ubunifu.

“Mchango wake utakumbukwa daima kwa vizazi na vizazi,”alisema Ndunguru ambaye pia aliwahi kuwa mwanafunzi wa Semzaba mwaka 1998 na baadaye kufanya naye kazi kuanzia mwaka 2001.

Leonia Thadei, mmoja wa wanafunzi wa Semzaba ambaye hivi sasa yuko mwaka wa pili, alisema atamkumbuka mwandishi huyo kwa ushirikiano na ukarimu wake kwa wanafunzi.

Mwanafunzi mwingine ambaye yuko mwaka wa tatu, Mohamed Athuman, alisema: “Wanafunzi waliopita mikononi mwake, wana bahati sana kutokana na kile walichopata kutoka kwake.”

Habari za kifo cha mtunzi huyo wa hadithi pia zilimstua katibu mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Godfrey Mngereza ambaye hata hivyo alisema sanaa yake itaendelea kuishi.

Mngereza alisema uandishi wake ulikuwa bora na kutokana na maudhui ya tamthilia ya “Ngoswe: Penzi Kitovu cha Uzembe”, ilionekana ni vema kitabu hicho kikaingizwa kwenye mfumo wa elimu.

“Alikuwa mwandishi, mwanamichezo mzuri na alikuwa bondia pia. Semzaba ni mwandishi ambaye ameondoka, lakini kazi zake zile ambazo tayari zimeshatoka zitaendelea kuishi,” alisema Mngereza.

“Hakuna asiyemjua Semzaba. Sanaa yake, itaendelea kuishi kwa kipindi kirefu zaidi.”

Mngereza alisema sanaa imepata pigo kubwa kwa kuondokewa na mtu muhimu katika ulimwengu wa uandishi wa tamthilia.

Alisema kulikuwa na michezo mingi ambayo aliigiza naye ukiwemo wa “Korogonzi” ambao ulionyeshwa jukwaani mikoa mbalimbali na baadaye nchini Ethiopia kwenye tamasha la sanaa.



ZeroDegree.
Kifo cha Mtunzi wa Tamthiliya ya Ngoswe Penzi kitovu Cha Uzembe chatikisa sanaa. Kifo cha Mtunzi wa Tamthiliya ya Ngoswe Penzi kitovu Cha Uzembe chatikisa sanaa. Reviewed by Zero Degree on 1/19/2016 12:38:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.