Loading...

Wanafunzi hewa 7,728 wabainika jijini Mwanza.



TUME iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela kufanya uhakiki wa wanafunzi hewa katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza imebaini kuwepo kwa wanafunzi hewa 7,728.

Wanafunzi hao waliisababishia serikali hasara ya Sh milioni 177. Wamebainika baada ya kufanyika uhakiki wa awamu ya pili.

Akiwasilisha taarifa hiyo jana kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), Mwenyekiti wa Tume hiyo, Waryoba Sanya, alisema tume yake ilitumia muda wa siku 28 kufanya uhakiki wake kwa kutumia hadidu za rejea mbili zilizochunguza na kubaini idadi halisi na isiyo halisi ya walimu na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika halmashauri ya jiji la Mwanza.

"Baada ya uhakiki wa kina tume ilibaini kuwepo kwa wanafunzi waliostahili na wasiostahili waliopelekewa fedha za mpango wa elimu bila malipo", alisema.

Alisema tume yake ilitumia takwimu zilizotumika hadi Desemba mwaka 2015 za kuwaletea wanafunzi fedha za elimu bila malipo, ambapo ilibaini kuwepo wanafunzi 102, 065, ambapo kati yao 75,002 walikuwa wanapokea fedha za elimu bila malipo kutoka serikalini.

"Tume ilitumia mbinu shirikishi katika kuifanya kazi hii, walimu wakuu wa shule zote za sekondari na msingi walijaza takwimu walizokuwa nazo kwenye kumbukumbu zao za Machi mwaka 2015 na kuhusisha idadi ya wanafunzi waliohamia, waliohama, waliofariki na waliofukuzwa shule tangu kipindi hicho", alifafanua.

Alisema katika kufanya uhakiki huo, tume ilitembelea shule 110 na kubaini wanafunzi 27,063 ndio wanaostahili kupelekewa fedha za elimu bila malipo.

"Kwa kuzingatia shule moja moja, tuligundua kuwa shule 56 zilikuwa zikiletewa fedha zilizozidi za mpango wa elimu bila malipo kwa kutumia idadi ya wanafunzi waliokuwa wamezidi idadi halisi ya wanafunzi waliokuwepo mwezi Desemba, 2015," alisema.

Aidha alisema tume ilibaini kuwa walimu 5,385 ndio waliokuwepo kwenye vituo vyao vya kazi na walimu 32 hawakuwepo kwenye vituo vya kazi kwa sababu mbalimbali na kuongeza kuwa kiasi cha Sh bilioni 1.9 kilikuwa kimetumika kwa ajili ya kulipia mpango wa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari kwa halmashauri ya jiji la Mwanza kuanzia Desemba 2015 hadi Agosti mwaka huu.

Mkuu wa Mkoa, Mongela alisema aliamua kuunda Tume hiyo ili kuondoa mkanganyiko uliokuwepo kati ya uongozi wa Chama cha Walimu (CWT) Wilaya na Taifa na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba, ambapo CWT ilipinga taarifa ya walimu na watumishi hewa iliyotolewa na uongozi wa jiji hilo.

Katika uhakiki wa awali, Kibamba alibaini kuwepo kwa wanafunzi hewa 13,000 na walimu hewa 13,000.

ZeroDegree.
Wanafunzi hewa 7,728 wabainika jijini Mwanza. Wanafunzi hewa 7,728 wabainika jijini Mwanza. Reviewed by Zero Degree on 12/22/2016 05:46:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.