Loading...

Wahitimu vyuoni ambao bado wanalamba fedha za mikopo wabainika.

VYUO vikuu 29 nchini vimejikuta matatani baada ya ukaguzi kubaini vina wanafunzi hewa 2,192 ambao kwa mwaka wa fedha 2015/16 pekee, wametafuna Sh. bilioni 3.85, baadhi yao wakiwa wanalipwa licha ya kuhitimu masomo miaka minne iliyopita.



Kutokana na hali hiyo, serikali imevitaka virejeshe fedha hizo ndani ya siku saba kuanzia jana na kwamba, madudu waliyoyabaini yamefanya sasa wapange kufanya ukaguzi wa hesabu za miaka ya nyuma katika vyuo hivyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alisema vyuo hivyo ni kati ya 31 vilivyofanyiwa ukaguzi kwa awamu ya kwanza kati ya 81 vilivyopo nchini.

Profesa Ndalichako alisema ukaguzi huo uliofanywa na kitengo cha ukaguzi wa ndani cha Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Akifafanua juu ya wanafunzi hao, Profesa Ndalichako alisema Julai 18, wizara ilitoa taarifa ya awamu ya kwanza ya ukaguzi ambapo wanafunzi 2,763 wa vyuo vilivyokaguliwa hawakujitokeza.

Alisema baada ya kutangaza majina ya wanafunzi hao kwenye vyombo vya habari na katika vyuo vyao, 571 walijitokeza kuhakikiwa katika vyuo 31 na mpaka timu hiyo inamaliza kazi, ilibaini wanafunzi hewa ni 2,192.

Alisema katika uhakiki huo, mbali na kushirikisha uongozi wa vyuo kutambua majina ya wanafunzi husika, pia walishirikisha viongozi wa madarasa wa wanafunzi husika.

Alisema viongozi hao wa madarasa, waliwatambua baadhi ya wanafunzi huku wengine wakiwa hawawajui.

Kutokana na hali hiyo, Profesa Ndalichako alisema: “Wakaguzi walikuwa wanarudi kwenye vyuo mara tatu tatu ili kuhakikisha wanafunzi hawa wanahakikiwa na kulikuwa na ushirikishwaji mkubwa, sasa kama yupo ambaye hakujitosa sasa, itabidi aanze upya kuomba mikopo,” alisema Profesa Ndalichako.

Waziri huyo aliongeza kuwa matokeo ya ukaguzi huo yameonyesha kuna umuhimu wa kukagua pia fedha zilizotolewa kwa wanafunzi hao kwa miaka ya nyuma kutokana na kile alichosema ni mtandao mkubwa ulio kwenye suala hilo.

Alisema kwenye baadhi ya vyuo, wakaguzi hao walibaini orodha ya majina inayotoka chuoni kwenda benki ili kuingizia wanafunzi fedha, ni tofauti na ile iliyo kwenye benki husika.

“Hiyo inaonyesha kuna mtandao mkubwa, lakini lazima tuchunguze hili na kwa sababu tunafanya kazi na Takukuru, mambo yataenda na kwenye maeneo mengine itabidi tuviachie vyombo vingine vya usalama kushughulikia,” alisema.

Alisema ili mwanafunzi apewe mkopo ni lazima matokeo yake yapelekwe bodi, lakini wamebaini vyuo vilikuwa vinafoji matokeo na kupeleka hata ya wale waliofukuzwa vyuo kwa kushindwa masomo ama kufariki na wengine waliohitimu masomo yao.

Alisema kwenye baadhi ya vyuo, wahasibu na maofisa mikopo wameshapewa barua za kujieleza ni kwanini wasichukuliwe hatua.

Waliohitimu 2013, wanaendelea kupata mkopo


Abubakari Msuya, ambaye ni Ofisa wa Takukuru anayeshiriki ukaguzi huo, alisema katika ukaguzi wao wamebaini kwamba, baadhi ya wanafunzi waliohitimu chuo mwaka 2013/14 wameendelea kupata mkopo.

Alisema walipochunguza akaunti zinazowekewa fedha hizo, walibaini kuwa ni za wanafunzi wenyewe kama inavyoonekana kwenye orodha ya shule.

“Tutakapoendelea na uchunguzi ndio tutatujua kama hizo fedha zinaishia kwao ama kuna watu wanakula nao,” alisema.

Kibao kwa waliodhamini wanafunzi

Katika hatua nyingine, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa (HESLB), Jerry Sabi, alisema ili kupambana na wadaiwa sugu, sasa bodi hiyo inatarajia kuanza kuwashughulikia wadhamini wa wanafunzi wanaodaiwa.

“Tumeshatangaza majina ya wanaoidawa, kinachofuata ni kwenda kwa wadhamini wao, tumefukua tukapata orodha yao na siku siyo nyingi tutawatangaza,” alisema.

Kwenye tangazo la bodi hiyo, lilisema baadhi ya hatua zitakazochukuliwa kwa wadaiwa sugu wa bodi hiyo ni pamoja na kutopata mikopo eneo lolote nchini, kutopata nafasi za kusoma ndani wala nje ya nchi na kutoruhusiwa kusafiri nje ya nchi.

Vyuo vinavyotakiwa kurudisha fedha


Katika orodha ya vyuo 31 vilivyokaguliwa, Chuo cha Mtakatifu Agustino (Saut-Mbeya) na Chuo Kikuu cha Biashara (CBE-Dodoma), havikuwa na wanafunzi hewa.

Kwa upande wa vyuo vimevyoongoza kwa kuwa na wanafunzi wengi, ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambapo wanafunzi waliostahili kupata mkopo ni 13,972, waliobainika kuwa hewa ni 350 na walilipwa Sh. milioni 703.43.

Kinachofuatia ni Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), ambapo wanafunzi waliotakiwa kupata mikopo walikuwa 16, 535 lakini walibainika 364, ambao walilipwa kiasi cha Sh. milioni 460.96.

Vingine ni Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph (SJUIT), waliopata mikopo 3,777, hewa 200, walilipwa Sh. milioni 408.85 na Chuo Kikuu cha Sokoine (Sua), waliostahili mikopo 6,227, hewa 235 walilipwa Sh milioni 387.62.

Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana Dodoma (SJUT), waliopata mikopo 2,577, hewa 164, walilipwa Sh. milioni 294.78, Chuo Kikuu cha Kimataifa Kampala (Kiu), waliopata mikopo 1,514, hewa 83, walilipwa Sh. milioni 172.96.

Chuo Kikuu cha Usimamizi wa Fedha (IFM), waliopata mikopo 3,625, hewa 85, walilipwa Sh. milioni 147.314, Chuo Kikuu cha Elimu Dar es Salaam (Duce), waliopata mikopo 4,486, hewa 84, walilipwa Sh. milioni 146.19 na Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji – (Mbeya-Teku) waliopata mikopo 2,146, hewa 47 walilipwa Sh. milioni 145.02. Wakati Chuo Cha Elimu ya Biashara (CBE-Dar es Salaam), waliolipwa mikopo 454, hewa 27, walilipwa Sh. milioni 65.64 na Chuo Kikuu cha Mzumbe (Mu), waliopata mkopo 3,295, hewa 29, walilipwa Sh. milioni 48.36 na Chuo Kikuu cha Kiislam (MUM-Morogoro), waliopata mkopo 1,122, hewa 30, walilipwa Sh. milioni 44.1.


Credits: Nipashe
ZeroDegree.
Wahitimu vyuoni ambao bado wanalamba fedha za mikopo wabainika.  Wahitimu vyuoni ambao bado wanalamba fedha za mikopo wabainika. Reviewed by Zero Degree on 8/18/2016 11:32:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.