Loading...

Undani wa sakata la serikali kuzuia ardhi aliyopewa Paul Makonda na mfanyabiashara jijini Dar

SERIKALI imesema eneo la ekari 1,500 alilopewa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Pual Makonda wiki iliyopita na Mkurugenzi wa Azimio Housing Estate, Mohamed Iqbal halimilikiwi kihalali na mfanyabiashara huyo.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alisema eneo hilo lililopo wilayani Kigamboni jijini, ni la serikali.

Alisema kwa kuwa ni la serikali, mfanyabiashra huyo hakuwa sahihi kulikabidhi kwa Makonda na kudai ni mali yake.


Lukuvi alisema atachukua hatua dhidi ya Iqbal, kwa kumdanganya Mkuu wa Mkoa.

Waziri huyo alisema analaani kitendo cha mfanyabiashara huyo kumdanganya Mkuu wa Mkoa huku akiwa anafahamu kuwa eneo hilo halikuwa lake bali ni la wananchi na serikali.

Alipofutwa jana kuzungumzia suala hilo, Makonda alisema: "Lukuvi ni Waziri, Makonda ni Mkuu wa Mkoa na serikali ni moja."

"Kwa hiyo, kuidanganya serikali ni sawa na kujidanganya wewe mwenyewe. Eneo ni la serikali, tutaendelea na mpango wetu wa kujenga viwanda vidogo vidogo kwenye eneo hilo."

Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Lukuvi alisema tayari kuna baadhi ya wananchi walikuwa wanaishi katika eneo hilo na idadi yao anayo na watahakikisha wanapata haki yao katika eneo hilo.

Alisema eneo litakalobaki litatumika kujenga viwanda kama ambavyo lilikuwa lengo la serikali hapo awali, kabla ya eneo hilo kuingia katika mgogoro.

"Huyo Mohamed Iqbal, lile eneo silake, ni la wananchi," Lukuvi alisema. "Na wizara ilikuwa imeshaanza kushughulikia kero hiyo, yeye mwenyewe ndiye aliyewashtaki wananchi mahakamani, lakini akashindwa kesi.

"Kibaya zaidi pamoja na kufahamu kwamba eneo si lake, aliendelea kumdanganya Mkuu wa Mkoa.

"Kwa hiyo nataka kuwaambia kuwa lile eneo ni la serikali, sisi wizara na serikali ndio tunalisimamia na tuta-‘take interest’ (simamia maslahi) za wananchi walioko pale, wapo wanaoishi pale.

"Serikali itasimamia maslahi yao kwa sababu tuna majina yao, lakini eneo ambalo limebaki litapangwa na kupimwa halafu tutalifanya eneo la viwanda kama ambavyo alitaka kufanya Makonda na hiyo ndio ndoto za Rais (John Magufuli) na ilikuwa ni ndoto yetu ya muda mrefu, lakini tulishindwa kutekeleza kwa sababu lilikuwa na kesi mahakamani.

"Iqbal aliwashtaki wananchi mahakamani yeye mwenyewe, lakini alishindwa kesi kwa sababu alishindwa ku-‘prove’ (kuthibitisha), nataka niwaambie kwamba lazima nimchukulie hatua kwa sababu mimi ndiye nina vielelezo vyote vinavyoonyesha kwamba alimdanganya Makonda, na niwaambie tu kwamba huyu ni mmojawapo wa wanaodanganya, lakini wapo wengine wanaofanya hivyo, tutawachukulia hatua."

Alisema lengo la serikali la kuweka viwanda katika eneo hilo liko palepale na kwamba kwa sababu tayari hukumu imeshatolewa lazima watekeleze.

Alisema si jambo baya kwa wananchi kujitolea ardhi kwa ajili ya shughuli za maendeleo, lakini ni vema kuwa makini na kitu unachotoa.

"Ni jambo la kawaida kutoa ardhi kwa ajili ya matumizi ya maendeleo, tumekuwa tukishuhudia hata huko vijijini, mtu anatoa eneo lake kwa ajili ya kujenga shule, lakini lazima utoe kitu ambacho ni cha kwako, siyo cha uongo," alifafanua zaidi Lukuvi.

Jumanne iliyopita, Makonda alikabidhiwa eneo na Iqbal, huku tajiri huyo akieleza sababu za kutoa ardhi hiyo ni kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli katika ujenzi wa viwanda.

Baada ya kukabidhiwa eneo hilo, Makonda alisema litajengwa viwanda vidogo vidogo na kulifanya kuwa kitovu cha maenedeleo ya viwanda katika mkoa wa Dar es Salaam.
Undani wa sakata la serikali kuzuia ardhi aliyopewa Paul Makonda na mfanyabiashara jijini Dar Undani wa sakata la serikali kuzuia ardhi aliyopewa Paul Makonda na mfanyabiashara jijini Dar Reviewed by Zero Degree on 2/28/2017 02:31:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.