Loading...

Lowassa alivyotikisa bungeni kwa siku 2

Waziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa 
Kwa siku mbili mfululizo, jina la aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa lilirindima bungeni wakati watunga sheria wakijadili hotuba za bajeti za Ofisi ya Rais (Tamisemi) na Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Jina hilo liliibua mzozo bungeni juzi wakati mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari alipohoji utendaji wa Waziri wa Habari, Dk Harrison Mwakyembe.

Nassari alisema Dk Mwakyembe, aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya Bunge, hakumuhoji Lowassa, ambaye aliihama CCM mwaka juzi na kujiunga na Chadema, katika sakata la mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura baina ya Tanesco na kampuni ya Richmond Development ya Marekani.

Nassari pia alisema katika sakata la uvamizi wa studio za televisheni za kampuni ya Clouds Media, Dk Mwakyembe hajamuhoji mteule wa Rais aliyeongoza uvamizi huo akiwa na askari wenye silaha za moto.

Suala hilo lilimfanya Mwakyembe aombe mwongozo na kueleza kuwa hawakuona umuhimu wa kumuhoji kwa kuwa ushahidi ulikuwa wazi, jibu lililosababisha kelele kutoka upande wa upinzani.

Dk Mwakyembe alionekana kama ameweka kiporo suala hilo na jana aliliibua.

Akichangia hotuba ya wizara hizo mbili jana, Dk Mwakyembe alisema wapinzani wanataka kumsafisha Lowassa na kuwashauri waliwasilishe upya suala hilo bungeni na yuko tayari kuvuliwa uwaziri ili alishughulikie.

“Mimi nimekuwa najiuliza ni ujasiri wa aina gani? wa kumkaidi Waziri Mkuu, wa kumkaidi Rais, ujasiri upi?” alihoji Dk Mwakyembe.

“Hivi mheshimiwa mwenyekiti umeona wapi ambako mawaziri hawaongozwi na kanuni ya kuwajibika kwa pamoja bungeni?

“Hii inaitwa collective responsibility (uwajibikaji wa pamoja) na si kwamba tumeiokota tu, ipo katika Katiba tena Ibara ya 53 (2) inasema ‘mawaziri chini ya uongozi wa Waziri Mkuu watawajibika kwa pamoja bungeni.”

Alisema wasipowajibika kwa pamoja bungeni wanaonekana kama waoga.

“Ah hawa si majasiri. Sasa nyie mkija kuunda Serikali, maana labda 2090 huko, bahati nzuri nitakuwepo, mtakuwa watu gani ambao mna Serikali moja na kila mtu anaongea la kwake?” alihoji.

“Si hivyo tu, Waziri Mkuu mwenyewe ambaye sisi tunafanya kazi chini yake anawajibika kwa Rais, kuhusu utekelezaji wake.”

Aliwataka wabunge kutowapotosha wananchi. “Mheshimiwa mwenyekiti mimi nashangaa, tunapenda kuongelea wenzetu. Nimemuona mheshimiwa kiongozi wa kambi ya upinzani alivyoingia, watu mpaka mikanda inalegea,” alisema.

“Wanatetemeka hapa, kimya, nidhamu, lakini leo sisi kumheshimu Waziri Mkuu wetu ambaye tuna wajibu wa kumheshimu.”

Richmond

Akizungumzia sakata la Richmond lililosababisha Lowassa ajiuzulu uwaziri mkuu Februari 2008, Dk Mwakyembe aliamua kujibu hoja za Nassari.

“Mheshimiwa mimi naelewa ni kazi ngumu kutaka kumsafisha Lowassa na kesi ya Richmond ilishakwisha. Na ndiyo maana sioni ajabu (kuwa ili) kusema aliyoyasema, ilibidi Nassari anywe pombe kwanza,” alisema.

“Nayasema haya kiongozi wa upinzani bungeni ajue kwamba tuna tatizo hilo. Mimi nawapongeza sana vijana wetu wa usalama waliokamata hiyo chupa na angeruhusiwa na hiyo chupa, huenda angeweza akatapikia hata rangi zetu za taifa humu ndani. Ingekuwa ni scandal (kashfa) kubwa.”

Alisema kuwa kazi ya kamati teule iliyoundwa na Bunge la Tisa ilikuwa kuchunguza na kutoa uamuzi.

“Tunapochunguza suala la kusikiliza ni upande mwingine, upo wakati wa maamuzi, ndiyo maana sisi tulikuja hapa, tukaleta kazi hapa, tukiwa na mashahidi zaidi ya 40 wakitusubiri nje,” alisema.

“Aliyetakiwa kuhojiwa hapa akajiuzulu. Unamlaumu Mwakyembe kwa hilo? Naomba msipotoshe umma kuwa hakuhojiwa, ahojiwe vipi? Unajua ni aibu?

“Sisi tulikuwa tumepata nyaraka za Serikali 104, tukahoji watu 75, tuliwauliza maswali 2,717 iko kwenye kumbukumbu rasmi za Bunge.

“Hatukuona sababu ya kumhoji Lowassa, tulikuwa na ushahidi wote. Mimi niombe, mwenyekiti kama kuna mtu yeyote hapa bado anakereketwa na kesi ya Richmond, alete hiyo kesi hapa kama hatujawanyoa kwa kipande cha chupa.”

Aliahidi kuwa siku ambayo mbunge yeyote atawasilisha suala la Richmond bungeni, atamuomba Rais ampumzishe uwaziri aweze kushughulikia hiyo kesi kikamilifu ili iishe moja kwa moja.

Kuhusu andiko lake la uzamivu kuhusu muundo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano ambalo Nassari alidai Dk Mwakyembe alikuwa na msimamo tofauti na CCM kuhusu idadi ya serikali, alisema alitoa kauli hiyo kwa kuwa alilewa.

“Watu ambao wanakesha miaka mitano kumtukana mtu kumuita fisadi, leo wanamkumbatia wanalamba na nyayo zake, ndiyo vigeugeu namba moja hao,” alisema.

“Halafu leo unajifanya kuja kumsafisha, huwezi kumsafisha madoa ya lami kwa kutumia kamba ya katani au maji. Lileteni hili suala hapa tulimalize,” aliongeza.

Kubenea aomba mwongozo

Kauli hiyo ilisababisha mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea kuomba mwongozo akitaka Dk Mwakyembe atoa ushahidi.

Alisema katika ripoti ya kamati ya Richmond, Dk Mwakyembe aliliambia Bunge kuwa mtu anaweza kujiuzulu kwa kuwajibika kwa kuwa yeye mwenyewe anahusika au kuwajibika kwa mambo yaliyofanywa na walio chini yake.

Kubenea alisema kwa mujibu wa kumbukumbu za Bunge, Dk Mwakyembe alisema Lowassa alijiuzulu kwa mambo yaliyofanywa na walio chini yake lakini jana aligeuka na kusema ana ushahidi wa asilimia 100 kwamba Lowassa alihusika na jambo hilo.

“Mheshimiwa Mwenyekiti naomba kwa idhini yako unipe muda niwasilishe hansard hapa kwenye Bunge hili kuthibitisha maneno ya Dk Mwakyembe ya mwezi Februari mwaka 2008,” alisema Kubenea.

Kubenea alisema pia Dk Mwakyembe aliliambia Bunge kuwa Nassari juzi alikuwa na konyagi aliingia nayo bungeni jambo ambalo si kweli.

“Tulikuwa na Nassari mchana kutwa na alikuwa amekuja bungeni na soda ambayo ilikuwa imewekwa kwenye chupa. Jambo hilo ninaweza kulithibitishia Bunge hili,” alisema.

Akijibu utaratibu huo, Chenge alisema kiti kimesikia kuwa Nassari aliingia na chupa hiyo maeneo ya Bunge na si ndani ya bunge.

Kuhusu Richmond, alisema sakata hilo lilikuwa ni uamuzi wa Bunge na iwapo kama mtu anataka kufufua hoja hiyo taratibu zao za kikanuni zipo wazi na kutaka alete hoja hiyo kwa taratibu zinazokubalika na Bunge lenyewe litaipima.

Akijibu hoja hizo, Dk Mwakyembe alisema andiko lake linazungumzia mfumo wa Serikali na kwamba yeye anapambana na udhalimu ndiyo maana anaumia zaidi watu wanapoleta mzaha.

Pia alishikilia kauli yake kuwa Nassari aliingia maeneo ya Bunge na chupa ya Konyagi.

“Mimi nilikuwa naona. Bwana mdogo (Nassari) asome tu akipata muda. Mtoto wa mchungaji yule ameingia hapa na kachupa ka pombe,” alisema.

“Kubenea na magazeti yao leteni kesi ya Richmond. Nawaomba chondechonde ileteni hapa. Mmekuwa na makubaliano ya kumsafisha, hamtaweza. Leteni kesi hapa.”

Akizungumza nje ya ukumbi wa Bunge, Nassari alisema maneno ya kuwa alifika na pombe bungeni ni ya uzushi tu baada ya wabunge wa CCM kuona wameshikwa pabaya.

“Si kuna vyombo vya usalama hapa? Walete ushahidi wa kunishika na pombe. Hayo ni maneno ya uzushi tu baada ya kuona nimewashika pabaya,” alisema Nassari.

“Mimi siwezi kumwamini tena Dk Mwakyembe hata leo nisikie akiniambia kuwa amefiwa na mkewe siwezi kuamini hadi nione maiti yake.”

Alisema hamuamini Dk Mwakyembe kwasababu ni mtu wa kubadilika katika kauli zake.
Lowassa alivyotikisa bungeni kwa siku 2 Lowassa alivyotikisa bungeni kwa siku 2 Reviewed by Zero Degree on 4/21/2017 02:04:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.