Loading...

Anna Mghwira avuliwa uongozi ACT Wazalendo


Wakati mkuu mpya wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira akitafakari jinsi ya kuanza majukumu yake mapya, chama chake cha ACT Wazalendo kimemvua uongozi na kumuongezea changamoto katika kutekeleza kazi zake.

Mghwira aliapishwa juzi na Rais John Magufuli kuongoza mkoa huo, ambao ni moja ya ngome ya vyama vya upinzani, hasa Chadema, chama ambacho mkuu huyo wa mkoa aliwahi kuwa mwanachama wake.

Mghwira, ambaye jana alikuwa safarini kuelekea kituo chake kipya cha kazi, anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Saidi Meck Sadiki aliyejiuzulu kupisha vijana wenye uwezo wa kwenda na kasi ya Rais.

Hata hivyo, kutekeleza majukumu hayo huku akitetea nafasi yake ya uenyekiti, kama atataka kuendelea itakuwa moja ya changamoto nane zitakazomkabili katika utendaji wake.

Changamoto nyingine ni siasa za ushindani, wahamiaji haramu, magendo, migogoro ya ardhi, ujambazi wa kutumia silaha, biashara ya mirungi na wafanyabiashara ndogondogo.

Lakini, changamoto anayoweza kuanza nayo ni ya kuvuliwa uenyekiti, nafasi ambayo juzi alisema ataendelea nayo.

Jana, ACT Wazalendo ilimteua Yeremia Mganja kukaimu nafasi hiyo, ikisema imezingatia ibara ya 17 ya katiba yake ambayo inatamka kuwa kiongozi wa chama atakoma kuendelea na madaraka yake iwapo atashindwa kutekeleza majukumu yake.

Kaimu Kiongozi wa ACT, Samson Mwigamba alisema kamati ya uongozi wa ACT ilikutana jana kutafakari uteuzi wa Mghwira kuona namna gani anaweza kutimiza majukumu yake kama mwenyekiti wa chama na mkuu wa mkoa.


“Baada ya kutafakari kwa kina na baada ya mashauriano baina yake na viongozi na kutumia katiba ya chama, (Mghwira) anakoma kuwa kiongozi kwa kuwa kutakuwa na mgongano wa majukumu na masilahi,” alisema Mwigamba. 

Hata hivyo, Mwigamba alisema Mghwira ataendelea kuwa mwanachama wa ACT Wazalendo.

Mwigamba alimpongeza Rais Magufuli kwa hatua ya kuvunja mwiko na kuchagua wapinzani katika nyadhifa za utumishi wa umma.

Mbali na kumpongeza, Mwigamba alimshauri Rais kuwa awe anafanya majadiliano na chama husika kabla ya kuteua ili kuondoa migongano isiyo ya lazima ndani ya vyama na jamii.

“Pamoja na kwamba Rais anayo mamlaka ya kuteua amtakaye, ni hekima uteuzi huo ukafanywa kwa kushauriana na viongozi wa vyama husika ambavyo anachukua wanachama wake,” alisema Mwigamba. 

Mwigamba alisema kamati ya uongozi ya chama hicho haijashangazwa na uteuzi huo kwa kuwa ilani ya ACT wakati wa uchaguzi mwaka 2015 ilidhamiria kuanzisha serikali ya mseto.

Mghwira anakuwa kiongozi wa pili wa ACT Wazalendo kuteuliwa na Rais Magufuli baada ya Profesa Kitila Mkumbo kuteuliwa kuwa katibu mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

“Kwa kuteua viongozi kutoka ACT inadhihirisha kuwa chama hiki kina viongozi makini na kwa maana hiyo inatufungulia njia kuwa katika nafasi nzuri ya kuchukua dola katika Uchaguzi Mkuu ujao,” alisema Mwigamba. 

Akizungumza na waandishi wa habari wakati akiwa njiani kuelekea mkoani Kilimanjaro jana, Mghwira alisema amelazimika kwenda haraka mkoani humo ili kukamilisha hatua za msingi.

“Kuhusu masuala yote ya chama nimeshazungumza na kiongozi wa chama ambaye aliridhia uteuzi wangu,” alisema Mghwira. 

Mghwira alisema atarejea baada ya wiki mbili jijini hapa kuzungumza na viongozi wa ACT Wazalendo masuala ya kichama.

Baada ya kumuapisha, Rais Magufuli alisema kuwa aliamua kumteua Mghwira, ambaye alikuwa mmoja wa washindani wake katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2015, kwa sababu amebaini kuwa ni muadilifu, mchapakazi na ana uwezo.

“Nimekuchunguza, nimejiridhisha una uwezo wa kuwatumikia wananchi. Wapo watakaokusema na kukuonea wivu. Wewe chapa kazi,” alisema Rais. 

Uaminifu na uchapakazi wake utakabiliana na mtihani wa ushindani wa kisiasa mkoani Kilimanjaro.

Hekaheka za kisiasa

Wakati akijiandaa kuanza majukumu yake mapya, Mghwira atatakiwa kujua hali ya kisiasa ilivyo katika mkoa huo ambao ni ngome ya wapinzani.

Nguvu ya upinzani inathibitishwa na takwimu za matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliopita wakati mgombea wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa alipopata kura 266,636 dhidi ya 167,691 za Magufuli katika majimbo tisa.

Mbali na takwimu hizo, upinzani unashikilia majimbo saba kati ya tisa, ukiwa na madiwani 145, vitongoji 910, vijiji 472 na mitaa 38.


“Tunachomsihi asije na ajenda ya kuua upinzani. Hili litamfanya akumbane na migogoro mingi. Kuna dhana ya Serikali ya CCM kukandamiza miradi tunayobuni, akiiga huko atapotea,” alisema Basil Lema, ambaye ni Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro. 

Katibu wa itikadi na uenezi wa CCM wa Moshi, Priscus Tarimo anasema haoni kama Mghwira atapata tabu kuuongoza mkoa huo kwa vile watu wake wana hekima na ni wastaarabu.

“Ila ajue anakuja mkoa ambao umekamatwa na upinzani. Afikirie ki-CCM lakini ajue kuna upinzani,” alisema. 

Migogoro ya Ardhi

Mghwira pia atakumbana na tatizo la ardhi katika mkoa huu wenye rutuba, kubwa likiwa ni mgogoro kati ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na wananchi.

Wananchi wa vijiji vya Sanya Station, Matindigani, Mtakuja na Chemka venye kaya zaidi ya 4,000, wamezuiwa na Serikali kufanya shughuli yeyote hadi ufumbuzi wa mgogoro huo utakapopatikana.

Migogoro mingine ni ya mipaka ukiwamo unaohusisha kijiji kilichopo katikati ya Kilimanjaro na Arusha.

Biashara ya wahamiaji haramu

Kilimanjaro pia imekuwa kitovu cha wahamiaji haramu kutoka Kenya wanaofanya kazi bila vibali na raia wa Ethiopia na Somalia wanaopita kwenda Afrika Kusini.

Biashara ya kupokea, kuwahifadhi na kusafirisha wahamiaji haramu ndiyo inayotikisa vijiji vya mpakani na Kenya katika wilaya za Moshi, Rombo na Mwanga.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini, kila mhamiaji hulipa kati ya Sh100,000 na Sh200,000 kwa ajili ya kuhifadhiwa katika nyumba za wenyeji wakati mawakala wakiwatafutia usafiri kwenda Mbeya.

Biashara ya magendo

Katika mambo ambayo Mghwira atakumbana na kazi ngumu ni usafirishaji mahindi, sukari na spiriti kwenda Kenya.

Wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakitumia njia zaidi ya 500 za panya katika wilaya za Rombo, Moshi Vijijini na Mwanga kupitisha bidhaa hizo.

Wakati bidhaa hizo hupelekwa Kenya usiku, zipo bidhaa nyingine zinazoingizwa kimagendo kutoka nchi hiyo, hasa mafuta ya taa.

Kushamiri uingizaji mirungi

Mbali na magendo, mkuu huyo wa mkoa pia atatakiwa kutafutia dawa biashara ya dawa za kulevya aina ya mirungi ambayo imekuwa ikiingizwa kutoka Kenya kwa kutumia pikipiki.

Mtandao huo wa uingizaji mirungi ni mkubwa ukihusisha baadhi ya mgambo na polisi wasio waaminifu ambao wamegeuza uingizaji huo wa mirungi kuwa mradi wa kuwapatia kipato.

Suala jingine ni ujambazi uliokithiri mkoani hapa ambao umekuwa ukitikisa. Ujambazi wa kutumia silaha, zikiwamo za kivita huku baadhi ya wahalifu wakisemekana kutokea Kenya.

Kwa takribani mwezi mmoja, kumetokea matukio ya uporaji wa kutumia silaha, ikiwamo SMG katika maeneo ya Tarakea na Moshi mjini na wakati mwingine kusababisha mauaji.

Wengi wanaofanya uhalifu huo, wanadaiwa kuwa ni wale wanaoachiwa kwa kushinda rufaa baada ya kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka 30 na kuachiwa.

Changamoto ya Machinga

Changamoto nyingine ni sehemu ya wafanyabiashara ndogondogo kuruhusiwa kufanya biashara katikati ya mji.

Hali hiyo imesababisha mji wa Moshi ambao ulikuwa ukiongoza kwa usafi nchini, kuporomoka kutokana na watawala kusita kuwagusa baada ya kauli ya Rais Magufuli kutaka wasibughudhiwe.

Mbali na machinga hao, wafanyabiashara katika masoko ya Mbuyuni, Soko la Kati na Manyema, hupanga bidhaa zao barabarani na kuzifanya zisipitike.


Anna Mghwira avuliwa uongozi ACT Wazalendo Anna Mghwira avuliwa uongozi ACT Wazalendo Reviewed by Zero Degree on 6/08/2017 11:48:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.