Loading...

Kiama kwa matapeli wa ajira za JWTZ kimefika

Mkuu wa Utumishi wa JWTZ, Meja Jenerali Harrison Masebo
JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limesema litamkamata na kumfikisha kwenye vyombo vya dola mtu yeyote atakayebainika kutoa rushwa kwa matapeli ili apate ajira katika jeshi hilo au Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Msimamo huo ulitangazwa jana jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Utumishi wa JWTZ, Meja Jenerali Harrison Masebo, wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema kumekuwa na wimbi kubwa la watu wanaotoa fedha ili vijana wao wapewe nafasi za ajira kwenye majeshi wakati wanaodai fedha hizo ni matapeli.

Alisema wananchi wanaotoa fedha ili wapate ajira na kuzikosa wamekuwa wakiwafuata viongozi wa Jeshi kutaka warejeshewe fedha walizotoa, hivyo kusababisha usumbufu mkubwa.

“Nafasi za kujiunga na mafunzo ya JKT hutolewa na Makao Makuu ya JKT kwa matangazo rasmi kupitia vyombo vya habari na siyo kupitia mitandao ya kijamii," alisema Jenerali Masebo. "Wananchi fuateni utaratibu huu.” 

Alisema yeyote atakayekwenda kulalamika kuwa ametoa fedha ili mtu wake ajiunge na Jeshi hilo, lakini amekosa, atahesabika kuwa ametoa rushwa hivyo atafikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.

“Ikumbukwe kwamba mtoa rushwa na mpokea rushwa wote ni wakosaji kwa mujibu wa Sheria," alisema na kutaarifu " (watu) muache kutumia njia zisizo sahihi katika kutafuta ajira au nafasi. 

"Ukitoa fedha itapotea na nafasi hutapata.” 

Aidha, Jenerali Masebo aliwatahadharisha wananchi kuhusu kuwapo wa kikundi cha watu wanaojifanya kuwa na uwezo wa kuwapatia vijana nafasi za ajira za moja kwa moja JWTZ.

Alisema kikundi hicho pia kimekuwa kikiwalaghai watu kuwa kina uwezo wa kutoa nafasi za kujiunga na JKT.

“JWTZ na JKT tumekuwa tukitoa ufafanuzi mara kwa mara namna ajira za JWTZ na nafasi za JKT zinavyopatikana," alisema. 

"Usajili wa vijana wanaotaka kujiunga na JKT huanzia ngazi ya vijiji, kata, wilaya hadi mkoa na waliofaulu usajili na vipimo vya afya hupewa fomu za kujaza.” 

Hata hivyo, pamoja na wananchi kusisitiziwa kuwa hakuna gharama zozote za kupata nafasi kwenye majeshi hayo, alisema, bado wapo wanaotoa fedha kama rushwa ili kupatiwa nafasi kinyume cha utaratibu.
Kiama kwa matapeli wa ajira za JWTZ kimefika Kiama kwa matapeli wa ajira za JWTZ kimefika Reviewed by Zero Degree on 6/08/2017 12:08:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.