Loading...

Ajira zaidi ya 10,000 zatangazwa kujaza nafasi za waliobainika kuwa na vyeti feki


Takriban miezi miwili na nusu baada ya Rais John Magufuli kupokea taarifa ya uhakiki wa watumishi wa umma, Serikali imetoa vibali vya ajira 10,184 kujaza nafasi zilizoachwa wazi na waliobainika kughushi vyeti vya elimu.

Serikali imesema vibali hivyo vinaziba pengo la walioghushi vyeti na kwamba, suala la ajira mpya bado liko palepale kama ilivyopanga kwenye bajeti ya Serikali ya mwaka huu wa fedha.

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika taarifa yake iliyoitoa jana kwa vyombo vya habari imesema imetoa vibali vya ajira hizo kwa mamlaka za serikali za mitaa, sekretarieti za mikoa, wakala za Serikali, taasisi na mashirika ya umma ili kujaza nafasi zilizoachwa na watumishi wa umma waliobainika kughushi vyeti hivyo.

“Mgawanyo wa vibali vya ajira umezingatia upungufu uliojitokeza baada ya kukamilika kwa uhakiki, vipaumbele vya Taifa kwa sasa na upatikanaji wa watumishi kutoka katika soko la ajira,” taarifa hiyo imemkariri Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki akisema katika kikao kazi na watumishi wa umma wa Wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam. 

Kairuki alisema utaratibu wa kukamilisha mgawo wa nafasi za ajira 4,816 zilizosalia unaendelea ili kuwezesha wizara na taasisi zingine zilizokamilisha uhakiki wa watumishi wa umma hivi karibuni kuajiri watumishi wapya kuziba nafasi zilizojitokeza.

Hiyo inamaanisha kuwa itakuwa imetoa jumla ya vibali vya kuajiri watumishi wapya 15,000 kuziba pengo lililosababishwa na kuondolewa kwenye orodha ya malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma waliobainika kughushi vyeti baada ya uhakiki.

Watumishi wa umma watakaoajiriwa kuziba nafasi hizo wanatarajiwa kuripoti kazini kuanzia Agosti.

Kairuki alisema utaratibu wa ajira mpya bado uko palepale, hivyo kuwataka wananchi kutokuwa na wasiwasi.

“Napenda nisisitize kuwa vibali tulivyovitoa leo ni vile vinavyoziba pengo la walioghushi vyeti. Naomba wananchi watambue kuwa suala la ajira mpya bado liko palepale kama Serikali ilivyopanga,” alisema Kairuki ambaye yuko katika ziara ya kikazi mkoani Dar es Salaam na jana alikuwa katika siku ya tatu aliyoitumia kukutana na watendaji na watumishi wa umma wa Wilaya ya Kigamboni, baada ya kuzungumza na watumishi wa umma wa Temeke na Mbagala. 

Lengo la ziara ni kukutana na watumishi wa umma na kusikiliza malalamiko, ushauri na changamoto zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi ili kuzifanyia kazi na kuleta mabadiliko katika utumishi wa umma nchini.

Aprili 28, Rais Magufuli alipokea taarifa ya uhakiki wa watumishi wa umma nchini wakati wa maadhimisho ya miaka 10 ya Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Akikabidhi taarifa hiyo kwa Rais Magufuli, Waziri Kairuki, alisema wizara yake iliagiza Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kuhakiki vyeti vya kidato cha nne, cha sita na vya ualimu.

“Jumla ya watumishi wa umma 435,000 walifanyiwa uhakiki wa vyeti vyao vya taaluma, watumishi 9,932 kati ya waliohakikiwa walikutwa na vyeti vya kughushi na vyeti vyenye utata. Vyeti 1,538 vilikuwa vikitumiwa na jumla ya watu 3,076,” alisema. 

Akihutubia baada ya kupokea taarifa hiyo, Rais Magufuli aliwataka watumishi hao waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi waondoke kazini mara moja na kuagiza mamlaka zilizowaajiri kukata mishahara yao.

Alisema kuwa kwa wale watakaobakia kazini, wakamatwe ili sheria ichukue mkondo wake ikiwamo kufungwa jela miaka saba.

“Mtu aliyeghushi vyeti hatuwezi kumsamehe. Wote wataondoka mara moja, mishahara yao ikatwe kabisa. Hao watumishi 9,932 wenye vyeti feki waache wenyewe kazi mara moja, watumishi wenye vyeti feki ambao watabaki kwenye ajira hadi Mei 15, wakamatwe wafikishwe kwenye vyombo vya sheria wafungwe hiyo miaka saba,” alisema. 

Alisema, “Wanaotumia cheti kimoja watu wawili, wasiwekewe mshahara ya mwezi huu, na kama wanajijua wajisalimishe, pia nikuombe Waziri utangaze mara moja nafasi za kazi 9,932 za watumishi wenye vyeti feki ambao wametakiwa kuondoka mara moja kazini ili zichukuliwe na watu wengine wenye vigezo.” 

Wakati Wizara ya Utumishi ikitangaza kujaza nafasi hizo 10,184 Mamlaka ya Mapato nchini(TRA) ilitangaza nafasi za ajira zaidi ya 400, Julai 4.

Tangazo lililotolewa na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma likiwataka Watanzania wenye sifa kutuma maombi yao kabla ya Julai 17.

Nafasi zilizotangazwa ni pamoja na idara ya rasilimali watu, wasimamizi wa mifumo ya mawasiliano, wanasheria na wahasibu.
Ajira zaidi ya 10,000 zatangazwa kujaza nafasi za waliobainika kuwa na vyeti feki Ajira zaidi ya 10,000 zatangazwa kujaza nafasi za waliobainika kuwa na vyeti feki Reviewed by Zero Degree on 7/13/2017 09:35:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.