Mkapa alivyozua mjadala baada ya kutumia neno hili kwenye mkutano wa hadhara
Kitendo cha Rais mstaafu Benjamin Mkapa kutumia neno wapumbavu kimeiibua Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ambayo imekilaani ikisema ni kejeli.
Wiki hii kwenye mkutano wa hadhara mjini Chato mkoani Geita, Mkapa akizungumza na wananchi alisema, “Kulingana na takwimu za Wizara ya Afya kuhusu maendeleo yaliyofikiwa ni wazi kwamba watu hao ni wapumbavu.”
Alisema hayo baada ya Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku ‘Msukuma’ kusimama awali na kueleza kuwa maendeleo yanayofanywa na Taasisi ya Benjamin Mkapa yanamkumbusha kauli ambayo Rais huyo wa Awamu ya Tatu aliwahi kuitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 alipowaita watu wanaopinga maendeleo kuwa ni wapumbavu.
Kauli hiyo imeifanya tume hiyo kujitokeza na kueleza kuwa ni ya kejeli kwa wananchi wenye maoni tofauti na yale ya uongozi wa nchi ulioko madarakani.
Taarifa ya tume hiyo kwa vyombo vya habari iliyosainiwa juzi na mwenyekiti wake, Bahame Nyanduga na kusambazwa jana inaeleza kusikitishwa kwake kusikia Mkapa akirudia maneno ya kejeli kwa Watanzania wenye maoni tofauti na yale ya uongozi wa nchi ulioko madarakani, kuwa ni wapumbavu na malofa aliyoyatamka Julai 10 akiwa Chato mkoani Geita.
“Matamshi haya hayapendezi kusikika kutoka kwa kiongozi wa kitaifa. Ni matamshi yasiyoheshimu maoni tofauti. Tume inaamini matamshi haya ni kinyume cha haki ya kila mtu kuwa na maoni tofauti. Pili yanapingana na kauli za viongozi kuwa kampeni za uchaguzi ziliisha na sasa tuungane tufanye maendeleo,” alisema Nyanduga na kutoa ushauri, “Tume inashauri viongozi wasijihusishe na matamshi ya kejeli au matusi kwani hayajengi utawala bora.”
Katika ufunguzi wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 kwenye Viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam alipokuwa akimnadi Dk John Magufuli wakati huo akiwania urais, Mkapa alitoa kauli kuwa wanaodai vyama vyao ni vya ukombozi ni wapumbavu na malofa.
Alisema Watanzania walikwishakombolewa na vyama vya Tanu na ASP na kwamba chama pekee cha ukombozi kilichobaki ni CCM, kauli ambayo ilipingwa na makundi mbalimbali wakiwamo wanasiasa na wasomi.
Mkapa alivyozua mjadala baada ya kutumia neno hili kwenye mkutano wa hadhara
Reviewed by Zero Degree
on
7/13/2017 08:56:00 AM
Rating: