Loading...

Ofisi ya Chama cha Mapinduzi [CCM] Mafia yachomwa moto


Watu wasiojulikana wameichoma moto ofisi ya Chama cha Mapinduzi tawi la Mshonzini iliyopo wilayani Mafia mkoani Pwani na kuteketeza mali mbalimbali za chama hicho.

Akithibitisha tukio hilo, Katibu wa CCM wilayani Mafia Mohammed Dhikiri amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Alhamisi Julai 13.

Dhikiri amesema moto huo umeteketeza kabisa ofisi hiyo pamoja na samani za ndani.

Amesema bado haijajulikana sababu za ofisi hiyo kuchomwa moto kwa kuwa wakati tukio linatokea hakukuwepo na viashiria vyovyote vya vurugu miongoni mwa wanachama.

Amesema bado halijafahamika ni nani aliyehusika na tukio hilo na kueleza kuwa wameliachia Jeshi la Polisi kuendelea na uchunguzi zaidi dhidi ya tukio hilo.

Awali akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Mbunge wa Mafia, Mbaraka Dau alisema vipo viashiria vinavyoonyesha kuwa alifika mtu asiyejulikana karibu na ofisi hiyo kisha kuwasha na kurusha kijinga cha moto kwenye paa la makuti la ofisi hiyo.

Dau amesema mtu huyo baada ya kutekeleza kitendo hicho aliondoka kuelekea kichakani kama ambavyo alama za nyayo za miguu yake zilivyoonyesha.

Amesema hilo ni tukio la kwanza kutokea wilayani humo kwa kuwa hadi linatokea hapakuwa na viashiria vyovyote vile vya kutokuwepo kwa Amani kati ya wanachama au viongozi.

Alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Rufiji, Onesmo Lyanga simu yake iliita bila kupokelewa.
Ofisi ya Chama cha Mapinduzi [CCM] Mafia yachomwa moto Ofisi ya  Chama cha Mapinduzi [CCM] Mafia yachomwa moto Reviewed by Zero Degree on 7/13/2017 06:30:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.