Majonzi yatawala wakati miili ya Wanajeshi 14 wa JWTZ ikipokelewa
Miili hiyo ilirejeshwa majira ya jioni na kupokelewa na umati wa askari wa JWTZ wakiongozwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi pamoja na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo.
Ni mara ya kwanza kwa wanajeshi wengi kiasi hicho wa JWTZ kuuawa katika misheni ya kulinda amani, kwa mujibu wa Jenerali Mabeyo aliyekuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari uwanjani hapo.
Miili hiyo ililetwa na ndege maalum ya Umoja wa Mataifa huku ikiwa imefunikwa bendera ya UN.
Baada ya kuwasili, kwa huzuni wanajeshi walianza kuchukua mwili mmoja baada ya mwingine na kuhamishia katika magari maalum yaliyokuwa yameandaliwa.
Kila mwili ulibebwa na wanajeshi nane wakati wa kuhamishia katika magari hayo kwa ajili ya kusafirisha kwenda kuilaza katika Hospitali Kuu ya Jeshi ya Lugalo, jijini.
Jumla ya magari saba yalitumika kubebea miili hiyo, kila moja ikibeba miili miwili na kusindikizwa na kundi la wanajeshi.
Akizungumza kabla ya kuanza safari hiyo ya kwenda Hospitali ya Lugalo, Dk. Mwinyi alisema miili hiyo inatarajiwa kuagwa Alhamisi katika viwanja vya Wizara ya Ulinzi, eneo la Upanga.
Pia alisema tukio la kuuawa kwa wanajeshi hao wamelipokea kwa masikitiko makubwa na kwamba wataendelea kuchukua tahadhari ili kuzuia kutokea kwa tukio kama hilo tena.
Kwa upande wake, Jenerali Mabeyo alisema tukio kama hilo ni la kwanza kutokea na kwamba hawajatetereka.
“Unavyolinda amani, lazima utegemee lolote, na tukio hili ni la kwanza katika kipindi cha miaka mitano," alisema Jenerali Mabeyo. "Hatuna hofu."
"Isipokuwa unaposhambuliwa, unajitazama umekosea wapi halafu unajirekebisha.
Aidha, mkuu wa majeshi alisema hali ya wanajeshi waliojeruhiwa ambao wako Kinshansa, DRC na nchini Uganda inaendelea vizuri na kwamba mmoja aliyepotea kati ya wawili amepatikana.
Kufuatia vifo hivyo, Rais John Magufuli ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu alituma salamu za rambirambi kwa Waziri Mwinyi, Jenerali Mabeyo, maofisa wote wa Jeshi na kwa familia zote za marehemu mwishoni mwa wiki iliyopita.
Katika salamu hizo Rais Magufuli alisema: “Nimepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kuuawa askari wetu kumi na wanne na wengine arobaini na wanne kujeruhiwa, na wawili hawajapatikana huko DRC wakati wakitekeleza majukumu ya ulinzi wa amani.
"Natoa pole sana kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na familia, (na) wakati tukisubiri taarifa kamili kutoka DRC niwaombe Watanzania tuwe na subira."Mungu wetu yuko pamoja nasi."
Taarifa ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres Ijumaa ilisema shambulio hilo ndilo baya zaidi kuwahi kutekelezwa dhidi ya walinda amani wa umoja huo katika historia yake miaka ya karibuni.Pia alielezea kusikitishwa na tukio hilo.
“Ningependa kueleza kusikitishwa kwangu na shambulio hilo lililotekelezwa usiku wa jana (Alhamisi) dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini DRC," alisema katika taarifa hiyo.
"Shambulio hilo lilitekelezwa kwenye kambi ya jeshi ya Semuliki, eneo la Beni katika mkoa wa Kivu Kaskazini.Taarifa ya UN ilisema pia wanajeshi watano wa Jeshi la DRC (FARDC) waliuawa kwenye shambulio hilo."
Majonzi yatawala wakati miili ya Wanajeshi 14 wa JWTZ ikipokelewa
Reviewed by Zero Degree
on
12/12/2017 12:05:00 PM
Rating: