Karaha ya usafiri mwisho wa mwaka yaanza Ubungo
Magari zaidi ya 10 yamezuiwa na Askari wa usalama barabarani kufanya safari za mikoani kwa ajili ya ukaguzi katika kituo kikuu cha mabasi cha Ubungo jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mwananchi, Mkuu wa Usalama Barabarani Ubungo, Said Ibrahimu leo Jumanne Desemba 12,2017 amesema wanaendelea na ukaguzi na kwamba magari yaliyozuiwa ni mabovu.
Katika kituo hicho cha mabasi idadi ya abiria imeongezeka kwa kiasi kikubwa chanzo kikielezwa kuwa ni kutokana na sherehe za mwisho mwaka.
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) jana Jumatatu Desemba 11,2017 kupitia taarifa kwa umma imetangaza kutoa leseni za muda mfupi katika kipindi cha mwisho wa mwaka.
Sumatra imewaalika wamiliki wenye mabasi ya ziada kuwasilisha maombi ya leseni za muda mfupi kwa ajili ya kuongeza huduma katika njia za mikoani zenye mahitaji zaidi kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka.
Mamlaka hiyo pia imewakumbusha wananchi wanaotarajia kusafiri kwa ajili ya mapumziko ya sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kupanga safari mapema ili kuepusha usumbufu unaotokana na changamoto za usafiri.
Karaha ya usafiri mwisho wa mwaka yaanza Ubungo
Reviewed by Zero Degree
on
12/12/2017 11:52:00 AM
Rating: