Loading...

6 washikiliwa mauaji ya polisi wawili mkoani Kigoma


WATU sita wanashikiliwa na polisi mkoani Kigoma, wakituhumiwa kuhusika na mauaji ya askari polisi wawili.

Askari hao waliuawa wakati wa operesheni ya kuwaondoa wafugaji katika maeneo ya hifadhi ya msitu wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma wiki iliyopita. Mkuu wa jeshi la polisi nchini, Inspekta Jenerali Simon Sirro akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nguruka na Uvinza wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, akiwa katika ziara ya kuangalia maafa na vifo vya askari hao alisema kuwa wote waliohusika na mauaji ya askari hao wataadhibiwa vikali kwa mujibu wa sheria.

Sambamba na hilo, mkuu huyo wa jeshi la polisi alisema pia polisi inafanya uchunguzi kuona mazingira ambayo mwananchi mmoja ambaye anaaminika kuwa ni mfugaji aliuawa katika vurugu hizo na kama itabainika askari walihusika hatua zitachukuliwa.

“Hakuna mtu yeyote mwenye haki ya kuua polisi au polisi kuua raia kila mmoja haki yake ya kuishi lazima iheshimiwe na kwamba polisi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama vinachunguza kwa makini chanzo cha vurugu na hatua za kuchukua,” alisema.

Pamoja na hilo alisema kuwa operesheni ya kuwaondoa wafugaji hao katika maeneo ya hifadhi na maeneo yalisioruhusiwa kwa ajili ya mifugo lililokuwa likiendeshwa na mamlaka ya ranchi za Taifa (NARCO) imesimamishwa ili kufanya tathmini ya yaliyotokea na namna bora ya kuiendesha bila kuleta madhara.

Mmoja wa wananchi katika mkutano huo, Hamad Kafunsi alisema kuwa ni lazima serikali itekeleze wajibu wake wa kulinda raia dhidi ya vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na askari.

Kwa upande wake, Mussa Uvinza alisema kuwa tangu kuingia kwa wafugaji kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa maarufu Wasukuma kumekuwa na mauaji ya mara kwa mara ya raia wanaookotwa mashambani huku vitendo vya kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wananchi ni tatizo ambalo limechukua nafasi kubwa na kusababisha vurugu kubwa baina ya wakulima na wafugaji.

Source: Habari Leo
6 washikiliwa mauaji ya polisi wawili mkoani Kigoma 6 washikiliwa mauaji ya polisi wawili mkoani Kigoma Reviewed by Zero Degree on 10/26/2018 12:05:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.