Loading...

Namba za gari la waliomteka Mo hazitambuliki


IMEBAINIKA kuwa namba za usajili zilizobandikwa kwenye gari linalodaiwa kutumika kwenye tukio la utekaji wa mfanyabiashara maarufu nchini na barani Afrika, Mohamed Dewji ‘Mo’ hazitambuliki kwenye mfumo wa bima.

Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) imesema upo mfumo unaoweza kubainisha mmiliki wa gari baada ya kutazamwa namba ya usajili, lakini kwa suala hilo TRA imewaachia Polisi kufanya uchunguzi.

Mo alitelekezwa alfajiri juzi kwenye viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam, ikiwa ni siku ya tisa tangu atekwe wakati akiingia kwenye Hoteli ya Kifahari ya Colloseum iliyopo Oysterbay kufanya mazoezi.

Kuachiwa huru kwa MO kulikuja siku moja baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro kuonesha hadharani picha ya gari aina ya Toyota Surf lenye usajili wa namba za kigeni za AGX 404 MC, namba ambazo uchunguzi umebainisha ni za Jiji la Maputo nchini Msumbiji.

Gari hilo lilikutwa limetelekezwa kwenye viwanja hivyo vya Gymkhana ndani yake kukiwa na silaha mbalimbali na safari hii likiwa na kibao cha namba za usajili, T 314 AXX za hapa nchini huku kwenye vioo kukiwa na namba za awali za AGX 404 MC.

Uchunguzi uliolenga kubaini kama namba hiyo ya hapa nchini imesajiliwa na TRA na endapo ipo kwenye mfumo wa malipo ya bima umebaini kutokuwepo kwa namba hiyo kwenye mfumo wa bima.

Mfumo huo wa Tira miss unawezesha kubaini kama gari husika limekatiwa bima au hapana na kama limekatiwa unaonesha ni aina gani ya bima, ya muda gani na lini imekatwa taarifa zinaweza kusaidia kugundua mmiliki wake halali.

Baada ya kuuliza katika mfumo huo kuhusiana na nambari hizo za T 314 AXX majibu yake yalikuwa; ”Hiki chombo cha moto hakina bima. Kata bima mpya, tii sheria bila shuruti.”

Hatua hiyo inaashiria kuwa huenda namba hizo ni bandia na zilitengenezwa na watekaji hao ili kuuhadaa umma wa Watanzania katika kutekeleza mpango wao huo.

Mfumo wa utambuzi TRA Hata hivyo gazeti hili lilipowasiliana na TRA ili kufahamu kama namba hiyo imesajiliwa na kama mmiliki wake anafahamika; mamlaka hiyo kupitia kwa Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi Richard Kayombo ilibainisha kuwa upo mfumo unaoweza kubainisha mmiliki halali wa namba ya gari kwa maana ya namba hiyo inaweza kuwa ni ya gari la nani.

Kayombo alisema,”kama gari limesajiliwa nchini basi namba ya gari ikipatikana tu inaweza kusaidia kumjua mwenye namba hiyo ni nani, wa wapi na hadi mawasiliano yake, ila kwa sasa kuhusiana na hili la tukio la utekwaji hatuwezi sema lolote hiyo ni kazi ya Jeshi la Polisi.”


Credits: Habari Leo
Namba za gari la waliomteka Mo hazitambuliki Namba za gari la waliomteka Mo hazitambuliki Reviewed by Zero Degree on 10/22/2018 02:50:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.